Mchungaji kizimbani madai ya Kuchunga ‘kondoo’ bila kibali

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 10:16 AM Apr 18 2024
Mchungaji wa Kanisa la Joy's Testimony of Christ Church, lililopo Kigamboni, Godgiven Mushindikwa akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matano likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria na kufanya kazi bila kuwa na kibali.
PICHA: HADIJA JUMANNE
Mchungaji wa Kanisa la Joy's Testimony of Christ Church, lililopo Kigamboni, Godgiven Mushindikwa akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matano likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria na kufanya kazi bila kuwa na kibali.

MCHUNGAJI wa Kanisa Joy's Testmony of Christ lililoko Kigamboni, Dar es Salaam, Godgiven Mushindikwa (52), raia wa Congo, amepandishwa kizimbani kwa mashtaka matano likiwamo la kufanya kazi za kichungaji bila kibali.

Mushindikwa alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, na kusomewa mashtaka dhidi yake na mawakili wa serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya na Ezekiel Kibona. 

Akisoma hati ya mashtaka, Kibona alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa makosa hayo Aprili 4, 2024.

Kibona alidai kuwa katika shtaka la kwanza, Mchungaji Mushindikwa anadaiwa  kuingia nchini kinyume cha sheria na Aprili 4, 2024 akiwa katika Ofisi za Uhamiaji zilizoko Kurasini, Dar es Salaam, alikutwa ameingia nchini bila kibali.

Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo na eneo hilo hilo, mshtakiwa kinyume cha sheria alikutwa akiishi nchini bila kibali ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.

Katika shtaka la tatu, Kibona alidai kuwa Aprili 4, 2024 mshtakiwa aliwasilisha  nyaraka za uongo katika ofisi ya uhamiaji ili apate nyaraka za kusafiria.

Ilidaiwa kuwa Mchungaji Mushindikwa katika tarehe hiyo na eneo hilo, aliwasilisha cheti za kuzaliwa na kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika ofisi za Uhamiaji, vyote vikiwa na jina hilo na alivipata kwa njia ya uongo.

Wakili Kibona alidai kuwa katika shtaka la nne, mshtakiwa akiwa katika ofisi za Uhamiaji akidaiwa kuwadanganya maafisa wa idara hiyo kwa kuwasilisha nyaraka za uongo ili kupata hati ya kusafiria.

Pia alidai mshtakiwa katika tarehe hiyo akiwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya  Congo, alikutwa akifanya kazi kama mchungaji katika Kanisa la Joy's Testmony Of  Christ, Kigamboni bila kibali.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikana tuhuma hizo na aliachiwa kwa dhamana  baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliotoka katika taasisi zinazofahamika. 

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 9,2024 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali.