MBUNGE wa Gairo, Ahmed Shabiby, ameiomba serikali kuweka tozo ya Sh.2, 000 kwa mwezi katika mitandao ya simu pamoja na mazao ili kuusaidia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea kujiendesha na kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/25, Shabiby alisema hatua hiyo itakuwa mkombozi kwa mfuko huo ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.
“Kwa hili wanaweza kulikubali au wasilikubali wengine watatukana kwenye mitandao, lakini acha watukane maana kuna watu hawapo duniani na hata mbinguni hawako. Wako katikati wanaelea, lakini siwezi kuogopa kwa sababu mtu atatukana.
“Ili kuinusuru bima ya afya, kuna umuhimu wa kuwapo chanzo ambacho kitakuwa cha uhakika katika kuchangia mfuko huo kwani wananchi wameshindwa kuchangia Sh. 30,000 kwa ajili ya bima ya CHF na hivi hatujajua hiyo bima kwa wote itakuwa na kiwango kipi,” alisema.
Shabiby alisema ikipangwa Sh.300,000 na Sh.60,000 kwa matibabu ya kawaida wananchi wa maeneo ya vijijini kuimudu itakuwa vigumu, hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kama inavyohitajika, hivyo ni wakati wa wananchi kujionea huruma ili kuokoa mfuko huo.
“Ukiangalia katika mipango ni kutaka kuwachangisha wananchi lakini namna ya kupata hii fedha itakuwa vigumu kama ilivyokuwa kwa CHF na leo hii ukiangalia wanufaika wa bima katika watanzania 100 ni watu wanane tu ambao wanalipa bima.
“Hii inaonyesha hatuna chanzo maalum cha kuchangia mfuko huu, kwakusaidia watu wasiyokuwa na uwezo wapate matibabu,”alisema.
Alitaja njia za kupata chanzo hicho cha uhakika kuwa ni pamoja na kuweka tozo katika mitandao ya simu ambayo inatumiwa sana nchini, zikiwapo zaidi ya laini milioni 72. Alisema ikiwekwa tozo ya Sh. 2,000 kwa mwezi kwa mwaka itakuwa Sh. 24,000 sawa na Sh. trilioni 1.728 kwa idadi ya laini hizo.
Mbunge huyo alishauri pia watumiaji wa mitandao hiyo wenye hadhi kama vile wabunge, wafanyabiashara, wafanyakazi kiwango kiongezwe hadi Sh.10,000 au 15,000 na kuunganishwa na kupatikana zaidi ya Sh.trilioni mbili.
“Pamoja na kuwapo kwa kiwango hicho, wananchi wa vijijini wasiwekewe ukomo wa matibabu kutokana na kuwa na kipato kidogo ambapo wamekuwa wakikosa matibabu na dawa za muhimu,” alisema.
Shabiby alisema viwango vingine vitafutwe hata kwenye mazao ambako kila kilogramu moja itatozwa Sh. moja au mbili kwa kuwa hata mkulima atanufaika na bima hiyo.
“Sasa kwa wale ambao hawana simu, hiyo inadhihilisha kuwa ni maskini wa kutupwa, hivyo hata hicho kiasi kidogo wasitozwe, atatibiwa kutokana na vyanzo hivyo vya mifuko,” alisisitiza.
VITUO VYA AFYA, ZAHANATI
Mbunge Shabiby alishauri zahanati za vijiji pamoja vituo vya afya vibinafsishwe akitolea mfano, nchi ya Korea Kusini ambako wamefanya hivyo kwa kuwekwa kwenye mfumo mmoja, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utolewaji wa huduma za afya.
Alisema kuwapo kwa mfumo huo wa ufuatiliaji wa vituo vyote vya kutoa huduma za afya, utasaidia kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika mfuko wa bima ikiwa ni pamoja na kusaidia ongezeko la wahudumu wa afya.
UTITIRI TOZO UVUVI
Mbunge wa Ilemela (CCM), Angelina Mabula, katika mchango wake aliomba serikali katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, itazame namna ya kuondoa utitiri wa tozo kwa wavuvi ili kudhibiti utoroshaji wa mazao ya samaki kwenda nje.
Mabula alisema ongezeko la ushuru wa mazao ya samaki kutoka Sh. 10 hadi Sh. 100 kwa kila kilo moja kunawaumiza wafanyabiashara na wavuvi, hali inayosababisha ongezeko la watu wanaouza na kusafirisha kwa magendo mazao hayo kwenda nje kinyume cha sheria.
Pia aliomba serikali kuongeza umakini katika kudhibiti wa utapeli mitandaoni kwa kuwa umezidi kushamiri hadi kwa viongozi, akijitolea mfano. Alisema licha ya mamlaka husika kusajili laini zote kwa alama za vidole, kuna watu walikuwa wakijitambulisha kwa jina lake na kutapeli watu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED