WAZAZI wa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru jijini Dodoma, wameshukuru Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa kujenga uzio wa shule hiyo ambao umesaidia kuondokana na muingiliano wa wafanyabiashara katika eneo hilo.
Shule hiyo ambayo ina miaka 96 ipo karibu na soko la Miembeni na uwanja wa Jamhuri jijini humo, ilikuwa ikizungukwa na wafanyabiashara kwenye eneo la shule kutokana na kukosa uzio, hali iliyokuwa ikisababisha wanafunzi kukosa utulivu wa masomo.
Wakitoa shukrani zake leo wakati wa hafla ya kukabidhi uzio huo,Mwenyekiti wa Kamati ya wazazi wa Shule hiyo, Aman Sadick na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Uhuru Rashid Gwazae wamemshukuru Mbunge huyo kwa ujenzi huo na kwamba ametatua kero iliyodumu miaka 96 ya maisha ya shule hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge Mavunde amesema awali kukosekana kwa uzio kulisababisha shule kuzungukwa vitendo vingi visivyo vya kimaadili katika eneo hilo huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo ya shule hiyo kongwe ya Uhuru.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED