Makonda awapa angalizo Wakuu wa Wilaya Arusha

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 09:16 AM May 11 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Picha: Beatrice Shayo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Misaille Musa, kuandika barua rasmi ya kuwataka wakuu wa Wilaya kutenga siku tatu za kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Makonda ametoa agizo hilo mkoani Arusha alipokuwa akisikiliza kero za wananchi katika oparesheni maalum aliyoiandaa ya siku tatu kwa ajili ya wananchi kupatiwa haki zao.

"Tukifika kwenye ziara Wilayani kwako, kwa mfano tukiwa Karatu Mkuu wa Wilaya atuambie huyu tulimsikiliza na kutatua kero yake kwa namna fulani na tumekwama eneo hili Mkuu wa mkoa tusaidie," amesema Makonda.

Amesema heshima ya Jiji la Arusha ipo  maeneo ya mijini tu, lakini ukiingia ndani Wilayani ni kama vile hakuna watu wa mipango miji, hivyo akawataka watendaji wote kuhakikisha kuwa wanasimamia ipasavyo sekta ya ardhi.

"Viwanja vinavyochangamkiwa ni vile vyenye hela hii sio sawa tunaanza ziara Mei 20 Mwaka huu nataka watendaji mkatende haki sio mnawaumiza hawa wananchi wa hali wa kipato cha chini katika kupata haki zao," amesema Makonda.