Makonda aitwa na Kamati ya Maadili CCM

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 09:17 AM Apr 22 2024
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
PICHA: CCM
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, leo anatarajia kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika ndani ya chama hicho, kuna uwezekano mkubwa Makonda akahojiwa na kamati hiyo baada ya kupewa barua ya kuitwa tangu Jumamosi iliyopita.

Aidha, chanzo chetu kimedokeza kuwa Makonda anatarajiwa kama ilivyopangwa kuhojiwa leo majira ya saa nne asubuhi ofisi za Makoa Makuu ya chama mkoani Dodoma na kamati hiyo ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana.

Chanzo hicho kilidokeza kuwa inawezekana Makonda katika kikao hicho akahojiwa kutokana na kauli anazozitoa ambazo zinakwenda kinyume na matakwa ya chama hicho.

Hata hivyo, chanzo hicho hakikufafanua zaidi kuhusu agenda za kikao hicho na kama kuna tuhuma zozote zinazomkabili Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha, ambaye alianza kutumikia mkoa huo katika siku za karibuni baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, Mkuu huyo wa mkoa, alipokuwa akiwasilisha salamu za mkoa wake, alidai kuwapo kwa viongozi wakiwamo baadhi ya mawaziri wanaolipa fedha watu kumtukana Rais Samia kwenye mitandao ya kijamii. 

Gazeti hili lilipomtafuta Makonda kuhusu wito huo, hakuthibitisha wala kukanusha.

Majukumu ya Kamati ya Maadili ya CCM ni kupokea taarifa za wanachama na viongozi wanaotuhumiwa kukiuka kanuni, taratibu na maadili kichama na kuzifanyia uchunguzi.

Kazi ya Kamati hiyo ni kuchunguza tuhuma za wanachama na viongozi kupendekeza adhabu au hatua za kuwachukulia wanachama na viongozi ambao wanakiuka maadili, wanaokwenda kinyume cha Katiba ya chama, miongozo na kanuni.

Pia kufuatilia mienendo ya viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kukiuka taratibu.

Katika kipindi cha uchaguzi kamati hiyo huchunguza mienendo ya wanachama ambao wanawania nafasi za uongozi na kutoa taarifa kwenye Sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.