Makada 44 CHADEMA wajitosa uchaguzi Moshi Mjini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:13 AM Jun 11 2024
Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa CHADEMA, Amani Golugwa.
Picha: Maktaba
Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa CHADEMA, Amani Golugwa.

MCHAKATO wa uchaguzi wa viongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Kaskazini umeshika kasi baada ya makada 44 kujitosa kugombea uongozi wa Jimbo la Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Jimbo la Moshi Mjini, lilikuwa likiongozwa na mgombea ubunge wa CHADEMA mwaka 2020, Raymond Mboya, Meya wa zamani wa manispaa hiyo.

Jana, Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa CHADEMA, Amani Golugwa, aliiambia Nipashe kwamba uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, patakuwa hapatoshi kwenye majimbo 35 ya mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara.

“Kwa Kanda ya Kaskazini, ndiyo tuko kwenye mchakato wa uchaguzi. Bado tuko katika ngazi ya majimbo na wiki hii tutakuwa na chaguzi kadhaa kwenye kanda yetu.

“Sasa hivi tunawafanyia interview (usaili) wagombea wote wa chama na mabaraza, tunawafanyia usaili. Tuko kwenye hatua ya uchaguzi ndani ya majimbo na ninavyozungumza jana (Jumapili), tumekamilisha usaili kwenye uchaguzi ambao tumeutangaza tayari, ni wa Moshi Mjini (Manispaa).

…Ndio Jimbo la kwanza tumeanza na tulikuwa na jumla ya wagombea 44 na wagombea 43 wameteuliwa. Mmoja hakukidhi vigezo. Hawa ni wagombea wa nafasi mbalimbali ngazi ya jimbo.” 

Wakati mtifuano huo ukiendelea majimboni, inaelezwa kuwa vigogo wanne wa kanda hiyo nao wananyemelea nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema anayemaliza muda wake.

Mei 30 mwaka huu, Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA aliandika kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, kuwa hatagombea tena nafasi hiyo.

Baada ya kauli yake makada wanne walioonyesha nia ya kumrithi wamo Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA)- Kilimanjaro na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Grace Kiwelu na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Yosepher Komba.

Wengine ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila na Gervas Mgonja, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Kanda ya Kaskazini.