Madudu ya kutisha yaibuliwa halmashauri

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:50 AM Oct 30 2024
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini madudu mbalimbali kwenye mamlaka za serikali za mitaa ikiwamo Sh. bilioni 61.15 kutokukusanywa na halmashauri 130 kutoka kwenye vyanzo muhimu vya mapato kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Miongoni mwa madudu hayo ni matumizi ya Sh. bilioni 5.16 kwa shughuli ambazo hazikukusudiwa, halmashauri kufanya malipo ya Sh. bilioni 7.42 bila kutumia stakabadhi za kielektroniki na madeni ya wazabuni Sh. bilioni 29.9 na ya watumishi Sh. bilioni 17.13. 

Sambamba na hayo, kamati pia imebaini kwamba katika halmashauri 47 zimetumia vibaya takriban Sh. bilioni 21.85 zilizokopeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya utekelezaji wa programu ya Kupanga, Kupima na Kurasimisha Ardhi, maarufu kama KKK.

Kutokana na madudu hayo, kamati imeitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na ofisi za makatibu tawala wa mikoa kufuatilia na kubainisha mashauri yote yaliyoko Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) yanayohusishwa na fedha zilizokusanywa kwa kutumia mashine za POS. Imesema Sh. bilioni 6.17 hazikuwasilishwa benki, hivyo kuagiza ziwasilishwe kabla ya Juni 30, 2025.

Akisoma jana bungeni taarifa ya kamati kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizokaguliwa hadi Juni 30, 2023, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee, alisema katika uchambuzi uliofanywa na kamati, imebainika kuwa kiasi hicho hakijakusanywa.

Mdee alibainisha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imeshindwa kukusanya Sh. bilioni 6.02 kutoka kampuni ya Yapi Merkez iliyokuwa inajenga reli ya kisasa (SGR) tangu mwaka 2021.

Pia alisema kamati inaitaka serikali ihakikishe halmashauri zote zinahuisha kanzidata ya walipakodi ili kupata taarifa sahihi na idadi kamili ya wafanyabiashara wanaostahili kulipa ushuru wa huduma na kuwasilisha kwa CAG kabla ya Machi 30, 2025.

“Serikali ihakikishe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakuwa na takwimu sahihi za mauzo ghafi ili halmashauri zikusanye kiwango sahihi cha ushuru wa huduma,” alisema.

MAWAKALA KITANZINI

Alisema kamati inaagiza serikali ihakikishe halmashauri 12 zinakusanya Sh. bilioni 5.65 kutoka kwa mawakala wa ukusanyaji mapato na kuchukua hatua stahiki kutokana na kutowasilisha mapato kwa mujibu wa mikataba yao.

Pia alisema serikali ihakikishe halmashauri zote zinafanya usuluhishi wa madai yote katika mfumo wa LGRCIS yenye thamani ya Sh. bilioni 45.02 ili kujua wadaiwa halali  na wadaiwa wasio halali ili kuondolewa katika mfumo kabla ya Machi 30, 2025.

STAKABADHI BANDIA

Alisema serikali ihakikishe halmashauri zote hazifanyi malipo yasiyo na stakabadhi za kielektroniki kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Utozaji wa Kodi, Sura ya 438 [iliyorekebishwa mwaka 2019).

“Imebainika halmashauri 64 zilifanya malipo yasiyo na stakabadhi za kielektroniki za Sh. bilioni 7.42 ikiwamo Halmashauri ya Singida ilipokea stakabadhi bandia zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 147,” alisema.

Pia alisema serikali ihakikishe halmashauri ambazo zilitumia Sh. bilioni 5.16 kwa shughuli ambazo hazikukusudiwa zirejeshe fedha hizo katika akaunti ya amana kabla ya Juni 30, 2025.

“Serikali ihakikishe halmashauri ambazo zilitumia Sh. bilioni 1.95 zaidi ya kiasi kilichowekwa katika akaunti za amana kurejesha kiasi hicho cha fedha kabla ya Juni 30, 2025,” alisema.

MADENI YA HALMASHAURI

Alisema kumekuwapo kwa madeni makubwa ya watumishi Sh.Bilioni 17.13 na wazabuni Sh.Bilioni 29.9 katika halmashauri 55 na kutaka serikali (Wizara ya Fedha) ilipe madeni yote yaliyohojiwa na CAG kwa hesabu zinazoishia Juni 30, 2023.

Alisema halmashauri 47 ambazo zinadaiwa Sh. bilioni 21.85 za mikopo ya programu ya Kupanga, Kupima na Kurasimisha (KKK) zirejeshwe Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Vile vile, alisema serikali iangalie upya utaratibu unaotumiwa na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika kutoza adhabu za ucheleweshaji pamoja na kufuata taratibu za kisheria ili kushughulikia hoja ya Sh. bilioni 32.07 inayotokana na faini/adhabu ya kutowasilisha michango kwa wakati.

MIRADI KUTOKAMILIKA

 Alisema kumekuwapo na tatizo la miradi kutokamilika kwa wakati na kusababisha kukosekana kwa tija ya uanzishwaji wa miradi hiyo pamoja na kuwakosesha wananchi manufaa ambayo yangepatikana iwapo miradi hiyo ingetumika kama ilivyokusudiwa.

“Bunge liazimie serikali ihakikishe inatenga bajeti ya kutosha ili miradi ambayo haijakamilika yenye thamani ya Sh. bilioni 206.89 inakamilika ili thamani ya fedha ya miradi hiyo ili kupatikana na iondoe dosari zote zilizobainishwa na CAG kwa miradi ambayo imekamilika lakini haijaanza kutumika ili miradi hiyo ianze kutumika kwa maslahi mapana ya wananchi,” alisema.

DCB IREJESHWE SERIKALINI

Alisema tathmini ya uwekezaji wa halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam katika benki ya kibiashara ya utendaji wa Benki ya Jamii ya Dar es Salaam (DCB) umekuwa ukishuka kila mwaka hadi kusababisha thamani ya hisa moja kufikia Sh. 140 kutoka Sh. 1000 wakati wa uanzishaji wa benki.

“Kuporomoka kwa thamani ya hisa na utendaji usioridhisha wa DCB umesababisha wanahisa zikiwamo Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zimewekeza Sh. bilioni 26.89 kupata hasara inayofikia Sh. Bilioni 16.7,” alisema.

Aliomba Bunge liazimie serikali kufanyika mabadiliko ya sheria yanafanyika ili Benki ya Jamii ya Dar es Salaam (DCB) iondoke kutoka benki binafsi na iwe katika orodha ya mashirika yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina.