Madereva walia gharama kujikimu, msururu wa malori wafikia 700

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:42 PM May 09 2024
Magari ya Mizigo, Mabasi na magari mengine madogo yaliyokwama kwa siku sita katika barabara ya Lindi-Dar es Salaam eneo la njia nne (Mikereng’ende) hadi Somanga yakitokea Lindi kuelekea Dar es Salaam yaanza kuruhusiwa kuendelea na safari.
Picha: Maktaba
Magari ya Mizigo, Mabasi na magari mengine madogo yaliyokwama kwa siku sita katika barabara ya Lindi-Dar es Salaam eneo la njia nne (Mikereng’ende) hadi Somanga yakitokea Lindi kuelekea Dar es Salaam yaanza kuruhusiwa kuendelea na safari.

MADEREVA wanaofanya safari za mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara na wengine wanaovuka mpaka kwenda nchi za Kusini mwa Afrika, wameegesha magari yanayofikia takribani 700.

Kutokana na barabara hiyo, kukatiza mawasiliano baada ya mvua kunyesha pamoja na kimbunga 'Hidaya' kilichotokea wiki iliyopita, kuleta athari, ikiwamo mafuriko.

Baadhi ya madereva, wamesikika wakipaza sauti zao kupitia Idhaa ya Kiswahili ya DW Radio, leo mchana, wakisema wanakumbwa na changamoto nyingi kama vile, gharama za kujikimu kila siku.

Mmoja wa madereva hao amesema, madereva wanalazimika kulipia ushuru wa Sh. 3,000 kila siku, kula chakula kinachouzwa kwa bei ghali, huku maji ya kunywa ya Sh. 1,000 yakiuzwa Sh. 2,000 hivi sasa.

Mahmoud Ismail, dereva wa lori, naye anasema ametelekeza gari na kuamua kuondoka, kutokana na kukosa fedha, kwa kuwa tajiri yake alipowasiliana naye, hana majibu yanayomfariji.

Aidha, takribani abiria 200 waliokwama waliokuwa wakisafiri, walilazimika kuvushwa kwa kutumia boti binafsi kwa gharama ya Sh. 5,000 hadi 20,000 kwa mtu mmoja.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema, leo, Alhamisi, Mei 9, mwaka huu, juhudi zinafanyika kuhakikisha mikoa ya kusini inafunguka.

"Naamini kabisa tulivyowaahidi Watanzania siku ya Alhamisi, tutarudisha mawasiliano, ni saa ngapi? Tutatoa taarifa baadae, kutokana na hatua za ujenzi zinavyoendelea," amesema Waziri.


CHANZO DW Radio