SIKU tano baada ya mwili wa askofu kukutwa unaning'inia kwenye kamba ofisini kwake, kumeripotiwa tukio lingine kama hilo, kiongozi wa kiroho nchini kudaiwa kufariki dunia kwa kujinyonga akitumia mshipi wake.
Rogassion Hugho (25), Frateri wa Kanisa Katoliki Shirika la Roho Mtakatifu Jimbo la Tanga, anadaiwa kufariki dunia juzi kwa kujinyonga katika nyumba yao ya malezi mkoani humo.
Inadaiwa kuwa frateri huyo alichukua uamuzi huo kutokana na kufeli mitihani ya kuingia hatua ya ushemasi wa kanisa hilo ambayo ni ngazi muhimu kabla ya kufikia sakramenti ya upadre. Hata hivyo, haijaelezwa na polisi ni lini mitihani hiyo ilifanyika.
Ni tukio linaloibua hoja "kulikoni watumishi wa umma?" Mei 16 mwaka huu, mwili wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist, Joseph Bundala, ulikutwa unaning'inia kwenye kamba ndani ya ofisi yake iliyoko katika kanisa hilo eneo la Meriwa, jijini Dodoma.
Iliripotiwa na Jeshi la Polisi kwamba ndani ya ofisi hiyo kulikutwa ujumbe kwamba askofu alichukua uamuzi huo kutokana na kuwa na madeni na mgogoro wa uendeshaji shule binafsi.
Wakati kuna hali hiyo, Mtaalamu wa Saikolojia, Saldin Kimangale, anaitolea ufafanuzi kwamba kasoro ya saikolojia ya akili haina mipaka ya wadhifa wala taaluma kwani inaangukia kwenye maradhi ya afya ya akili.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi jana kwa simu, alithibitisha kutokea tukio hilo, akieleza kuwa frateri anadaiwa kujinyonga juzi kwa kutumia mshipi wanaojifunga kiunoni watumishi wa kanisa hilo wa ngazi husika.
Alieleza kuwa frateri huyo anadaiwa kujinyonga katika nyumba yao ya malezi ya Magamba alimokuwa anaishi.
"Tukio hili ni la kweli lilitokea jana (juzi). Amejinyongea kwenye makazi yao ambayo wanajiandaa kuwa mapadri. Sababu ya mwanzo inayosemekana ni kwamba kawaida hufanya mitihani kwenda hatua nyingine, sasa akawa amefeli.
"Ninasikia hakukubaliani na hiyo hali ya kushindwa, akapata msongo wa mawazo na akaona njia bora afanye hivyo. Amejinyonga kwa kutumia kamba hizi wanazojifunga kiunoni (mshipi)," alieleza Kamanda Mchunguzi.
Ni matukio ya vifo vyenye utata vya viongozi wa dini. Aprili 12, 2022, mwili wa Paroko wa Parokia ya Mt. Yohanne Paul II, Mbezi Mshikamano, Francis Kangwa ulikutwa katika tangi la maji nyuma ya nyumba ya mapadre wa Shirika la Missionaries of Africa iliyoko Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.
Wasaikolojia tiba wanasema kinachochangia uamuzi wa kujiua ni ugumu wa maisha na kushindwa kufikia malengo. Daktari, mtumishi wa Mungu, Rais na yeyote hawana kinga dhidi ya magonjwa ya akili na kuumwa magonjwa hayo hakutegemei kiwango cha uchamungu au wadhifa.
Mwanasaikolojia Tiba, Saldin Kimangale, katika mazungumzo na mwandishi jana kuhusu matukio hayo ya viongozi wa dini kudaiwa kujinyonga, alisema kumekuwa na matukio kadhaa ya watumishi hao wa kiroho kukatisha uhai wao, huku sababu zikitajwa ugumu wa maisha na kushindwa kufikia malengo.
"Bila shaka hizi ni sababu za kuwezesha mazungumzo yaendelee na kufunga kurasa za mijadala. Asilimia takriban 60 ya Watanzania wanaishi kwenye umaskini uliotopea, achilia mbali kufikia malengo mbalimbali.
"Ukweli ni kuwa nyuma ya mtu kukatisha uhai kuna mengi tusiyoyajua, yeyote anayekatisha uhai hakuanza kukatisha uhai wake siku ile aliyokamata kifaa cha kukatisha uhai na kukatisha, bali ni mchakato umeanza siku kadhaa nyuma, hata miezi, hata miaka," alisema.
Mwanasaikolojia Kimangale kutoka Kituo cha Somedics Polyclinic Heath Centre, Upanga, jijini Dar es Salaam, alisema ifahamike kuwa daktari, mtumishi wa Mungu, Rais na yeyote hawana kinga dhidi ya magonjwa ya akili na kuumwa magonjwa hayo hakutegemei kiwango cha uchamungu au wadhifa.
“Huu ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine, yanampata mtu yeyote maadam yupo kwenye vihatarishi. Linapokuja suala la "mtumishi wa Mungu" inaleta shida zaidi kwa sababu wao ndiyo hutarajiwa wawe na uvumilivu, subira na uthabiti zaidi na pia wawe na mbinu bora zaidi za mawasiliano na stadi za kutatua changamoto na matatizo mbalimbali kuliko watu wengine kwa kuwa jamii inawategemea," alifafanua.
Alisema dhana hiyo ya kuchukuliwa kuwa "anapaswa kuwa hivi" ndiyo inayowafanya pengine wasizifikie huduma kwa dhana kuwa wataonekana ni dhaifu au hawana imani na uchamungu.
Alisema watumishi wa Mungu kama wanadamu wengine wanapitia yaleyale wanayopitia watu wa kawaida ikiwamo aibu, hatia na kujihisi kushindwa.
"Ni vyema kada hii itazamwe upya tena kimfumo, anasema Mwanasaikolojia Kimangale. Janga la watumishi wa Mungu halina tofauti sana na janga la wanaume wanaokabiliwa na miiko inayowafanya wasilie na kutafuta msaada, sasa iwapo mtumishi ni mwanamume basi janga lake linakuwa kubwa zaidi.
Sababu walizozitoa zina maana kubwa sana kwao, jamii lazima iziheshimu na kuzitumia kama angalizo, ugumu wa maisha na kutofikia malengo kwa mtu mmoja si lazima iwe na maana sawa na mtu mwingine. Ili tuwasaidie ipo haja ya kuwasikiliza na kuwasaidia kutatua changamoto zao."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED