Dk. Mpango ataka idara za afya kuwezeshwa kutambua magonjwa yasioambukiza

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:22 AM May 10 2024
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philipo Mpango.
Picha: Julieth Mkirire
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philipo Mpango.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philipo Mpango ameiagiza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa ( TAMISEMI), kuziwezesha idara za afya kuanzia ngazi ya mkoa hadi kijiji, ziweze kuimarisha mifumo ya kutambua magonjwa yasiyoambukiza ili kudhibiti magonjwa hayo yasiendelee kuleta athari kwa jamii.

Makamu wa Rais, Dk. Mpango ametoa agizo hilo mjini Kibaha kwenye  uzinduzi wa Kampeni ya Mtu ni Afya  kitaifa, awamu ya pili iliyobeba ujumbe unaosema 'Mtu ni Afya'.

Amesema ili kufanikisha kampeni hiyo  Wizara  ya Afya na TAMISEMI,  wanatakiwa kufanya utafiti, ufuatiliaji  na udhibiti wa magonjwa hayo kwa kuhakikisha wanaendesha kampeni mbalimbali zinazolenga kuchochea mabadiliko kwa jamii, serikali za mitaa kuongeza uwezo wa kujenga mitaro, uzoaji wa taka kwenye maeneo yao na udhibiti wa taka ngumu.

Akizungumzia tatizo la ugonjwa wa kisukari, Dk. Mpango amesema  miaka ya 1980 ni asilimia moja tu ya wagonjwa walikuwa na tatizo la kisukari na asilimia tano ya wagonjwa wenye shinikizo la damu  lakini kwa sasa  kati ya watu 100,  tisa wana shinikizo la damu, na kati ya watu 100, 25 wana ugonjwa wa kisukari  na kwamba magonjwa yasiyoambukiza yanachangia asilimia 33 ya vifo.

Awali akimkaribisha  Makamu wa Rais, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema kampeni  ya awamu ya pili inajikita katika huduma za kinga, usafi wa mazingira na hali ya vyoo nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani una vituo vya kutolea huduma za afya 475 ambavyo kati ya hivyo hospitali ya Rufaa moja na hospitali zenye hadhi ya  Wilaya 12 na vituovya afya  50 na zahanati 388.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo ukiambatana na kutoa zawadi kwa maeneo  yalifanya vizuri kwenye eneo la Usafi, Halmashauri hadi Kijiji ambapo Mkoa wa Iringa uliibuka mshindi wa jumla kwa kupata zawadi ya gari.