DIWANI wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo amesema kero zilizosalia katika kata yake zitatatuliwa kwa wakati huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano pale wanapohitajika.
Tumike, ametoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa hadhara aliouandaa kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Alisema kwa kipindi alichokuwapo madarakani kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Segerea Bonna Kamoli wamefanikiwa kutatua changamoto kadhaa ikiwamo ya barabara.
"Barabara ya kwenda Zahanati ilishatengenezwa kwa kiwango cha zege, kimebaki kipande kidogo nacho kiko tayari kwenye mpango wa kumaliziwa mwaka huu.
“Ile ya kutoka Kinyerezi hadi Bonyokwa mpaka Kimara tayari mkandarasi yuko ‘site’ (kazini). Mvua itakapoisha ataanza kazi. Kuna barabara ya kutoka Masia, Kanisa Katoliki mpaka Baa Mpya iko katika mpango wa kujengwa.
“Lakini pia ya kutoka Segerea kwenda Bonyokwa tayari imejengwa mita 700 kwa kiwango cha lami na kipande kilichobaki kimeingia katika bajeti ya mwaka 2024/25 nacho kitamaliziwa mpaka kufika mwakani barabara nyingi zitakuwa zimejengwa,” alisema Tumike huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliofurika eneo hilo kupokea salamu zake. Sambamba na hilo, amewataka wananchi kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 itakapoanza kutolewa ili kujikwamua kimaisha.
“Mikopo muda si mrefu itaanza kutolewa, hvyo niwaombe mchangamkie mjiunge katika vikundi, fungueni akaunti benki mkajisalili ili iwe rahisi kupata mkopo. Tatizo kinamama wengi hawataki kufuata huo utaratibu ndiyo maana wanaangukia katika mikopo ya kausha damu,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED