MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash amezindua Oparesheni Mapinga 'tokomeza migogoro ya ardhi' katika kata hiyo ambayo itafanyika kwa siku tano.
Oparesheni hiyo inafanywa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Kamishna wa ardhi Pwani na wataalamu wa Sheria kutoka Mahakama na Halmashauri ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Shule ya Msingi Tambani kata ya Mapinga, Okash amesema kambi ya kusikiliza migogoro itakuwa hapo kwa siku tano.
Amesema Oparesheni hiyo imeanza katika kata ya Mapinga ambayo inaongoza kwa migogoro ya ardhi baadae itaenda Makurunge na Fujatosi ambazo wananchi wake wamekuwa na malalamiko ya migogoro ya ardhi isiyokwisha.
"Tumeona tuwafuate wananchi kwenye maeneo yao yenye migogoro, katika siku hizi tulizotenga kuwasikiliza kuna wakati tutatembelea maeneo yanayolalamikiwa tukiwa na wataalamu na kusikiliza pande zote na baadae utatuzi utafanyika," amesema.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Shukrani Kyando amesema ameungana na Mkuu wa Mkoa katika Oparesheni hiyo lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro iliyopo na kutoa ushauri kwa wananchi kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika Oparesheni hiyo wamempongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua hiyo ambayo itawasaidia kupata elimu na kitatuliwa migogoro yao kwa kufuata taratibu.
Katika siku ya kwanza ya Oparesheni hiyo watu zaidi ya 50 walijitokeza kuwasilisha kero zao ambapo idadi kubwa waliojitokeza ni wale waliouziwa maeneo ambayo tayari yana hati miliki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED