DC Mboni atoa ufafanuzi waliodaiwa kupewa adhabu na watumishi Msalala kisa ushuru

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 09:32 AM May 10 2024
MKUU wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita

MKUU wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita amelaani kitendo kilichofanywa na watumishi watano wa halmashauri ya Msalala kitengo cha ukusanyaji wa mapato ambao wameonekana kwenye kipande cha vitendo kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kikionyesha wakitoa adhabu kwa wananchi wanaodaiwa kukwepa kulipa ushuru wa mazao.

Mhita akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya simu akiwa safarini amesema,kitendo walichokifanya watumishi hao sio cha kiungwana na sio maelekezo ya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kukusanya mapato kwani kinakiuka haki za binadamu.
 
Alisema, tukio lilitokea Mei 02,2024 katika viwanja vya makao makuu ya Halmashauri ya Msalala kwa kuwapa adhabu ya kuruka kichura chura, kugaragara, kuwabebesha mataili pamoja na kuwamwagia maji, na kitendo hicho kilifanywa majira ya usiku muda wa kazi ukiwa umeisha.
 
Aidha alisema, baada ya serikali ya wilaya kuiona video hiyo mtandaoni walilazimika kuchukua hatua ya kuwakamata na kuwafikisha vyombo vya sheria na Mei 07,2024  waliachiwa kwa dhamana na sasa wamewasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuhuma zinazo wakabili.
 
Mhita alisema, watumishi hao walipaswa kutoa elimu wakati walipowamakata wananchi hao na sio kujichukulia sheria mkononi na kuwapatia adhabu walizotoa, kazi zetu zina miongozo, taratibu na kitendo hicho hakuna aliyefurahishwa nacho.
 
Hata hivyo amewataka watumishi wa halmashauri zote za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama kufanyakazi kwa kuzingatia sheria nasio kujichukulia sheria mkononi na upelelezi unaofanywa na jeshi la polisi utakapokamilika watumishi wote watano watafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo.