Daktari ataka wanaorudia uhalifu kupimwa afya akili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:14 AM May 10 2024
Wanaorudia uhalifu kupimwa afya akili.
Picha: Maktaba
Wanaorudia uhalifu kupimwa afya akili.

DAKTARI Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk. Godwin Mwisomba, amesema kuna haja ya kupima afya ya akili kwa wanaotenda matukio ya uhalifu na kuyarudia.

Aidha, amesema si jambo la kawaida kwa binadamu kurudia kosa alilofanya na baadhi kupewa adhabu na kutojutia kosa, jambo linaloonyesha kuna uhusiano mkubwa kati ya uhalifu na ugonjwa wa akili.

Bingwa huyo amefafanua hayo jana katika mada iliyohusu uhusiano kati ya magonjwa ya akili na uhalifu kwenye ukurasa wa kijamii mtandaoni Usalama Tv.

“Utafiti ulifanywa katika moja ya magereza huko Afrika Kusini, ulijumuisha watu 280 na hawa watu walikuwa wafungwa jinsi tofauti. Utafiti ulisema magonjwa ya akili yana uhusiano na kurudia kufanya uhalifu.

“Walichogundua zaidi ya theluthi ya watu hao, takribani 82, walikuwa na matatizo mbalimbali kama ya akili. Wengine wana wasiwasi mkubwa, sonona.

“Kuna sababu za kisayansi zinaonyesha wanaorudia uhalifu wana matatizo, changamoto na magonjwa ya akili. Kwa nini? Ukiangalia kuna vitu vitano. Kwanza, ubongo wa gamba la mbele ambao unaweza ukasema umepungua.

“Inapokuja mhemko, yeye anaweza akafanya kitu chochote. Uwezo  wake wa kufanya uamuzi kwamba uamuzi huu si sahihi, kwa sasa haupo. 

“Anawaza labda kuiba ili akanywe pombe, haoni tatizo. Ila  sisi tunalaumu tukio, yeye nafsi yake laumu haipo,” amesema Dk. Mwisomba.

Amesema jamii hulaumu tukio lililotendwa bila kufahamu iwapo kuna hitilafu ya ubongo kwa mtenda uhalifu, huku akisema sababu ya pili ya vitendo hivyo ni husababishwa na tatizo la ubongo kushindwa kuhimili hisia.

“Kuna mwitikio wa kihisia, mfano nipite nikamkanyaga mtu na nikahisi na nikamwambia samahani. Lakini utakuta mtu anayefanya uhalifu, hisia zake hazipo au imepungua, hata akipiga mtu ngumi na anamuumiza anaona kawaida,” amesema.

Amesema kwa hali ya kawaida, binadamu kupitia sehemu hiyo ya ubongo ‘amida’, kuna mfumo unaozuia uchokozi, uhalifu na kumpa mtu woga kutenda matendo yaliyo kinyume na jamii anayoishi.

“Kwa watu kama hawa wakiletwa kwa wataalamu kama sisi tunajua namna ya kumpa ushauri na mafunzo. Kwa sababu watu kama hawa hawawezi kuchangamana na jamii kuliko na sheria, utaratibu na yeye hawezi kufuata miongozo, hatambu hana woga.”

Bingwa huyo amesema pia katika ubongo kuna mfumo wa zawadi na adhabu, akisema wanaotenda vitendo vya uhalifu na kutojilaumu, mfumo wao upo katika kiwango cha juu.

“Utakuta yeye muda mwingi atakata hali yake ya kujisikia vizuri iwepo muda wote. Hastahimili hali. Mtu wa kawaida kama mfumo wako upo vizuri ukiwa na kiu ukinywa maji, unajisikia vizuri. Lakini hawa wasio na mfumo mzuri hata anywe maji hajisikii vizuri.

“Utakuta mtaani anashindwa kuishi, kila siku yuko polisi. Kuna vitu haviko sawa katika ubongo,” amesema.

Amesema kuna hatua za kufanya, akisema watu walio na rekodi ya kurudia vitendo vya uhalifu, wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi, ikiwamo ambao wamo katika magereza.

“Kwa wenzetu mtu kama huyu anaweza kupelekwa vitani, lakini kwenye jamii huku atasumbua. Tushirikiane kulishughulikia suala hili pamoja. Tuwatambue watoto wenye kasoro kiakili, ili tuanze mapema kuwafundisha.

“Hawa watu wakiingia kwenye mfumo wa haki jinai, itatumika fedha na rasilimali ya umma katika kuwahudumia watu hawa. Kwa hiyo wenzetu wanatumia utafiti na kusaidia kufanya uamuzi.

“Hii itaipunguzia gharama serikali kwa sababu kuna ambao watapata tiba na wakabadili kabisa tabia. Kuna magonjwa yanaanza utotoni, tunasema huyu mtoto mtukutu, baadae wanakuja kuwa wanajihusisha na uhalifu.

“Tunaweza kuwafikia katika familia na kutoa elimu, wengine ni tabia. Mazingira yanaathiri, labda katika familia wapo wanaotumia dawa za kulevya, watoto wanayabeba, wanaona ukatili kwa baba dhidi ya mama, chanzo mtoto mkatili ni makuzi aliyokulia,” amesema Dk. Mwisomba.