CAG abaini kiini wafungwa kurudia makosa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:55 AM Apr 19 2024
Wafungwa.
PICHA: MAKTABA
Wafungwa.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini kiini cha wafungwa wengi kurudia makosa wanapotoka gerezani.

Anakitaja kiini hicho katika ripoti yake ya ukaguzi wa ufanisi kwa mwaka 2022/23, iliyowasilishwa bungeni Jumatatu.

Ni ripoti inayotolewa kipindi ambacho kumekuwa na matukio ya wafungwa, wakiwamo wanaoachiwa kwa msamaha wa Rais, kurudia kufanya makosa wanaporejea uraiani, hata kuibua maswali “wanafundishwa nini gerezani?”

Katika ukaguzi wake, CAG Charles Kichere, amesema serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha programu za urekebishaji wafungwa kwa kuanzisha Kitengo cha Huduma za Urekebu wa Wafungwa chini ya Jeshi la Magereza Tanzania.

Vilevile, Jeshi la Magereza lilianzisha gereza la shule ya ufundi, Ruanda - Mbeya na gereza la vijana, Wami - Morogoro, na kuanzisha Stashahada ya Sayansi ya Urekebu kwa Maofisa Magereza katika Chuo cha Mafunzo ya Urekebu Tanzania.

CAG anataja maeneo yanayohitaji maboresho zaidi kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha wafungwa wanaorudia makosa kwa wastani wa asilimia 1.5 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023.

Anasema ukaguzi ulibaini ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa kwa wastani wa asilimia 1.5 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, licha ya mipango ya urekebu. 

“Hali hii inaonesha kuwa wafungwa zaidi wanarudi kwenye kufanya uhalifu. Kiwango cha kurudia kufanya makosa kilikuwa hakiendani na muda wa wafungwa gerezani. Wafungwa wengi zaidi walio na hukumu fupi walirudia makosa,” CAG anaeleza.

Kati ya mwaka 2019 na 2023, hali ya wafungwa waliorudia kufanya makosa ni asilimia 59.22, walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya mwaka mmoja; asilimia 24.65 walikuwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitatu.

“Asilimia 10.14 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka mitatu hadi mitano; na asilimia 3.09 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka mitano hadi 10,” alisema.

Aidha, asilimia 0.37 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 10 hadi 15; asilimia 2.22 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 15 hadi 20; asilimia 0.32 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 20 hadi 30; na asilimia 0.01 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 30.

KIINI CHA TATIZO

CAG anasema hali hiyo ilisababishwa na ukosefu wa mitaala na miongozo ya magereza kwa ajili ya uendelezaji rasmi wa mipango ya urekebu; uainishaji na utengano wa wafungwa kujikita kwenye jinsia na umri pekee; miundombinu isiyotosheleza ya uainishaji; shughuli za msingi za gereza kuamua uainishaji; na ukosefu wa sera na miongozo ya uainishaji wa wafungwa.

Pia, anataja kukosekana kwa mipango rasmi ya kuunganisha wafungwa wanaotarajia kukamilisha vifungo vyao.

CAG anafafanua kuwa ukaguzi wake ulibaini kuwa licha ya kuwapo programu za urekebu, hakukuwa na mpango rasmi wa kuwaandaa wafungwa wanaokaribia kukamilisha muda wao wa kifungo ili kuwaandaa kukabiliana na jamii watakayoenda kuishi ikiwemo changamoto kadhaa zinazoweza kuwapata katika kipindi hicho.

“Kukosekana kwa mfumo huu maalum wa kuwaandaa wafungwa, kunasababisha wafungwa kuachiwa bila kuandaliwa, hivyo kuwapa ugumu wa kupata huduma za jamii na misaada mbalimbali na kuchangia ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa,” CAG anawasilisha hoja yake.

Katika ripoti hiyo, CAG anabainisha kuwa kwa mwaka 2023 pekee wafungwa 3,262, walirudia makosa baada ya kutoka gerezani, wengi wao wakiwa ni walioachiwa huru baada ya kutumikia vifungo vifupi.

Pia, anaeleza, ukaguzi wake ulibaini uainishaji wa wafungwa katika magereza saba aliyotembelea unajikita zaidi kwenye jinsia na umri pekee, masuala mengine kama asili ya kosa, historia ya uhalifu na umuhimu wa urekebishaji hayazingatiwi.

“Ukaguzi pia ulibaini wafungwa na maabusu waliwapo katika magereza ambayo yalipangwa na kujengwa kwa ajili ya maabusu pekee.

“Hali hii ilisababishwa na miundombinu usiyotosheleza ya kusaidia uainishaji wa wafungwa na kutokuwapo sera na miongozo ya uaninishaji wafungwa,” CAG anasema.