Aliyeshtakiwa kwa mauaji Tanga, ana kesi ya unyang'anyi wa silaha Moshi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:15 PM Apr 19 2024
Wa kwanza kushoto, ni Eben Mwaipopo, mshtakiwa wa kwanza kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, na wa pili ni mshtakiwa mwenzake, Fredrick Mkwembe, wakiwa Mahakama ya Wilaya ya Moshi jana, muda mfupi kabla ya kuanza kwa usikilizaji wa mashahidi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wa kwanza kushoto, ni Eben Mwaipopo, mshtakiwa wa kwanza kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, na wa pili ni mshtakiwa mwenzake, Fredrick Mkwembe, wakiwa Mahakama ya Wilaya ya Moshi jana, muda mfupi kabla ya kuanza kwa usikilizaji wa mashahidi.

SHAHIDI muhimu wa Jamhuri katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili Eben Mwaipopo (27) na Fredrick Mkwembe au ‘Samora white,’ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Moshi, kwamba washtakiwa hao licha ya kupora bastola aina ya Norinco kwa mfanyabiashara maarufu wa Moshi, Denis Swai, walikuwa wakikabiliwa na kesi nyingine ya mauaji Mkoa wa Tanga.

Shahidi huyo wa upande wa mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Benedicto Petro kutoka Tanga, alikuwa akitoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi, akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Kambarage Samson anayesaidiwa na Imelda Mushi na Amina Mkayala.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Ruth Mkisi anayesikiliza kesi hiyo namba 231 ya mwaka 2022, shahidi huyo alidai kuwa washtakiwa hao walichukuliwa na maofisa wa Polisi Kilimanjaro kutoka Tanga, Juni 6 mwaka 2022, ambako walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya mlinzi wa shamba la mkonge.

Mfanyabiashara Denis Swai, aliibiwa silaha hiyo Juni 28 mwaka 2017 katika eneo la Soweto, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika kosa la kwanza la unyang’anyi wa kutumia silaha, ambalo ni kinyume na kifungu cha 287 (A) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Mwaka 2019, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba bastola aina ya Norinco, yenye thamani ya Sh.350, 000 za Tanzania, risasi 27 zenye thamani ya Sh.75, 600 na fedha taslimu paundi 30,000, sawa na Sh. milioni 79, 650,000 na mashine ya kupima damu yenye thamani ya Sh.100, 000.

Waliiba pia, Televisheni moja yenye thamani ya Sh.1, 200,000 mali ya Denis Elirehema Swai, na wakati huo huo kuwaweka chini ya ulinzi, Idda Denis Swai na Daniel Shayo na kuchukua mali hizo.

Wakati kosa la pili linalowakabili, ni kukutwa na mali inayosadikika kuwa ya wizi, ambayo ni kinyume na kifungu 312 (1) (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Mwaka 2019.

Katika ushahidi wake, Mkaguzi huyo wa Polisi, alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza (Mwaipopo), alikamatwa na maofisa wa Polisi katika Kituo cha Mabasi cha Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, Januari 25 mwaka 2018 na silaha aliwaeleza makachero wa Polisi kwamba iko Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.

Aliendelea kudai kuwa, Machi mosi mwaka 2018, walianza safari kwenda kuitafuta iliko silaha hiyo, na waliikuta ikiwa kwenye begi la mshtakiwa wa kwanza kwenye chumba alichopewa na shemeji yake, Ritha Godliving Makule.

Aidha, alidai kuwa walipofanya upekuzi waligundua kuwa bastola hiyo yenye usajili 47012895, yenye rangi nyeusi haikuwa na magazine (kifaa kinachohifadhi risasi).

Wakati mshtakiwa wa pili, Fredrick Mkwembe (Samora White), yeye alikamatwa  Januari 27 mwaka 2018 akiwa katika shughuli zake za bodaboda eneo la Bonite, Moshi.

Baada ya kutoa ushahidi huo, kuliibuka mabishano ya kisheria kati ya Mwaipopo na shahidi, huku Mwaipopo akitaka mahakama iruhusu apewe maelezo ya shahidi huyo ili ayatumie kumhoji.

Baada ya mvutano huo na upande wa mashtaka kujibu mapingamizi hayo, Hakimu Mkuu Mkisi, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 6 mwaka huu, mahakama hiyo itakapotoa uamuzi wake kuhusu mapingamizi yaliyojitokeza na kuendelea na usikilizaji wa kesi hiyo.