ACT yakemea kura feki katika uchaguzi

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:39 AM May 10 2024
Makamu wa Kwanza wa Rais  Zanzibar, Othman Masoud Othman
Picha: Maktaba
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman

CHAMA cha ACT Wazalendo kimekemea matumizi ya kura feki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ambazo kimesema zinawanyima wananchi haki ya kupata viongozi wanaowataka kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yao.

Aidha, kimependekeza kuwapo kwa uwazi na ushirikishwaji katika uzalishaji, utunzaji na usambazaji wa karatasi za kupigia kura ili kudhibiti kura feki kwenye uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Chama hicho taifa ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais  Zanzibar, Othman Masoud Othman,  amesema hayo wakati akizungumza na wazee wa chama hicho mkoani Kigoma.

Wazee hao wamemweleza kusikitishwa na kushamiri kwa matumizi ya  kura feki katika uchaguzi, wakiituhumu tume hiyo na  vyombo vingine vya serikali kuhusika ili kukipa ushindi chama tawala.

Othman amesema anafahamu hujuma zinazofanyika katika uchaguzi ikiwemo matumizi ya kura feki na kuwasihi wanaofanya vitendo hivyo kuacha kwani chama hicho kitaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzikomesha.

Amesema chama hicho kinapendekeza  wajumbe  waliopo wajiuzulu ili wapya wapatikane kwa utaratibu uliowekwa kwenye sheria pia kuwapo kwa uwazi na ushirikishwaji katika uzalishaji, utunzaji na usambazaji wa karatasi za kupigia kura ili kudhibiti kura feki kwenye uchaguzi.

 "Tatizo letu halijawahi kuwa jina la tume, tatizo letu ni muundo ambao unaifanya tume isiwe huru. Mabadiliko ya muundo wa Tume ya Uchaguzi yanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya wajumbe wa tume hiyo. 

“Wajumbe wa sasa  kuendelea ni  sawa na mtu yuleyule anajiita kuwa ni mtu mwingine kwa sababu tu amevaa nguo tofauti,” amesema.

Othman pia amekutana na kuzungumza na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma,  Joseph Mlola, na kuwapongeza  viongozi wa dini kwa mchango wao katika kuliombea na kuliunganisha taifa.

Pia amemshukuru Askofu huyo kwa  kukipongeza chama hicho kutimiza miaka 10 na kumhakikishia kuwa rai yake kwa chama ya kuwa sauti ya wasio na sauti itazingatiwa.

Amemweleza Askofu Mlola kuwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo   kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kuwa  wameshawaandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali mwinyi wa Zanzibar.

"Mpira uko kwao kufanyia kazi masuala ambayo ACT Wazalendo imeyasisitiza hasa mageuzi katika mfumo wa uchaguzi na haki Zanzibar kwa sababu iwapo masuala hayo yasipofanyiwa kazi, ACT Wazalendo itatekeleza uamuzi wake wa kujitoa," amesema.