Kambi ya matibabu ya siku tisa, 300 wakutwa na kisukari, presha

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:38 PM May 10 2024
Mkurugenzi wa Elimu Bridge Words Dk. Fahdy Hemed aliwasilisha maada Katika hafla ya kuwaaga madaktari bingwa
Picha: Halfani Chusi
Mkurugenzi wa Elimu Bridge Words Dk. Fahdy Hemed aliwasilisha maada Katika hafla ya kuwaaga madaktari bingwa

KATI ya watu 1,050 waliopimwa Katika kambi ya matibabu bure iliyofanyika katika Hospitali ya Istiqama Magomeni mkoani Dar es Salaam 300 wamekutwa na matatizo ya kisukari na presha.

Kambi hiyo ilifanywa na jopo madaktari bingwa sita kutoka Ujerumani kwa kushirikiana na wa hospitali hiyo na kudumu kwa siku tisa na kutamatika jana.

Hayo yamesemwa leo  na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Abdalah Mohamed  Katika hafla ya kuwaaga madaktari hao ambapo viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya walihudhuria. 

Alisema katika oparesheni hiyo wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 45 na tayari wameruhusiwa huku wengine 25 wakiendelea na matibabu chini ya uangalizi wa Hospital.

"Katika kambi hii tumewafikia wagonjwa mbalimbali, Presha na kisukari 300, wenye matatizo ya mifupa 200, Sikio, Pua na Koo 150, Figo 100 madaktari hao pia walibaini kuna wagonjwa wengi wa saratani lakini kwa bahati mbaya wataalamu  wake hawakuwapo tunataraji kambi ijayo watakuja" aliahidi  

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Afya Katika hafla hiyo,  Mratibu wa Tiba Utalii na Mratibu wa Tiba Nje ya Nchi Dk. Asha Mahita, aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo kuratibu kambi na kusaidia kuwapatia matibabu  watanzania 1,050.

"Tunawashukuru sana kwa kushirikiana ninaomba mwendele hivihivi isiwe tu Dar es Salaam ikiwezekana tuzunguke nchi nzima. Huduma za afya ni gharama kwa bahati mbaya wengi hatujui thamani ya afya, ifike mahali tuzingatie ushauri wa wataalamu ili kuepukana na maradhi yanayoweza kuzuwilika" alishauri

Alisema anatamani mbali na matibabu hayo elimu itolewe kuhusu mfumo wa maisha na vyakula akisistiza Istiqama ni taasisi ya muda mrefu ina vitu vingi vya kusaidia wananchi.

Mkurugenzi wa Elimu Bridge Words Dk Fahdy Hemed alisema alisema lengo la kambi hiyo lilikuwa kuwasaidia wagonjwa wasio na uwezo wa kifedha kupata matibabu ya kibingwa.

"Kambi nzuri sana mwitikio umekuwa mkubwa, hatukutegemea watu wagonjwa wamefika kwa wingi, safari ijayo tutajipanga zaidi kufanya mambo makubwa, tumefanya hivi pia kuiunga mkono Serikali na Wizara ya Afya" alisema 

Aliitaja kisababishi cha magonjwa hayo kwa wengi waliofika Katika kambi hiyo kuwa ni pamoja na kutofanya mazoezi, na mfumo wa maisha na vyakula akisistiza vingi tunavyokula havijengi afya.

"Tunahitaji madaktari wetu waendane na  teknolojia ya sasa kama ilivyo kwa wenzuetu wa Ujerumani, lakini tayari mpaka sasa nimeshapewa ofa ya kupeleka madaktari kwenda kusoma nje ya nchi kwaajili ya kuongeza ujuzi" alisema