Balozi aomba Mkabata wa Kimataifa wa Geneva uzingatiwe

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 04:05 PM May 09 2024
Balozi wa Uswiss nchini, Didier Chassot.
Picha: Mtandaoni
Balozi wa Uswiss nchini, Didier Chassot.

BALOZI wa Uswiss nchini, Didier Chassot amesema ukiukwaji wa Sheria ya Kimataifa ya Utu uliomo katika Mkataba Kimataifa wa Geneva, unachangia watu kuteseka katika nchi mbalimbali zenye vita.

Amesema, ipo haja ya kuchunguza vitendo vya uhalifu chini ya sheria hiyo ya kimataifa, hasa uhalifu wa kivita, na kuwafikisha mahakamani wale wanaoshukiwa kufanya uhalifu.

Balozi huyo amesema hayo jijini Dar es Salaam, akizindua mjadala kuhusu utu, ulioandaliwa na ubalozi wa Uswiss ukishirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

"Sheria ya Kimataifa za Utu (IHL) iliomo katika mkataba huo ikiheshimiwa na kila mmoja, migogoro na vita inayoendelea kutokea duniani inaweza kupungua. Hivyo ni vyema mataifa yote yajitafakari na kuchukua hatua ili kupunguza mizozo inayoleta vita," amesema Chassot.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Red Cross Tanzania, Hilary Ngude katikati akichangia mada katika mjadala huo. Kulia ni mwanafunzi Joseph Masangula na kushoto ni Meja Sebastian Mwakalindile.

Amefafanua kuwa sheria zilizomo katika mkataba huo zimeendelea kuokoa mamilioni ya maisha yanayotishiwa na mamia ya mizozo duniani kote na kuwaunganisha tena maelfu ya wanafamilia waliotengana.

"Mateso ya watu yanayotokana na kukiukwa hasa kwa Sheria ya Kimataifa ya Utu (IHL), ambayo ziko katika mkataba huo, ni makubwa, hivyo, kila taifa lihakikishe inaheshimiwa na kutekelezwa," amesema. 

Amesema, mkataba huo sasa umetimiza miaka 75 na kwamba alitarajia kwa kipindi hicho chote mataifa yangetambua umuhimu wake na kuepuka vita, au kulenga na kuumiza raia wasio na hatia.

"Kila nchi ina wajibu wa kuheshimu, kusimamia au kuchukua za  kuhakikisha Mkataba wa Kimataifa wa Geneva ambao sasa imetimiza miaka 75 unaheshimiwa kote duniani," amesema.

Msomi wa mwaka wa nne Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joseph Masangula amesema, vita vinavyoendelea sehemu mbalimbali duniani na kuumiza watu wasio na hatia ni ishara kwamba mkataba huo hauheshimiwi.

"Vita inaendelea katika nchi mbalimbali za Afrika na hata nje ya Afrika, watu wanakimbia nchi zao, wengine wanaumizwa, lakini Sheria ya Kimataifa ya Utu iliomo katika mkataba huo inakataza kuumiza raia wasio na hatia kwenye vita," amesema Masangula.

Amesema, mkataba huo una sheria mbalimbali ikiwamo hiyo ambayo inaelekeza kuwa katika vita, mashambulizi yasielekezwe kwa raia au kwenye makazi yao, na kwamba dunia imekuwa ikishuhudia  jinsi zinavyokiukwa na kusababisha madhara au vifa kwa raia.

 

Baadhi ya wadau wakifuatilia mjadala huo.