Mkuu wa Ujasusi Israel ajiuzulu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:58 PM Apr 22 2024
Mashambulizi ya anga yateketeza majengo katika Jiji la Gaza, Israeli mnamo Oktoba 8, 2023.
Picha: Mahmud Hams/AFP
Mashambulizi ya anga yateketeza majengo katika Jiji la Gaza, Israeli mnamo Oktoba 8, 2023.

MKUU wa Idara ya Ujasusi nchini Israel, Meja Jenerali Aharon Haliva amejiuzulu, ikiwa ni hatua ya kuwajibika kwa kushindwa kuzuia shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Hamas, Oktoba 7, 2023. Jeshi la Israel limethibitisha.

Meja Jenerali Aharon Haliva ni Afisa wa kwanza wa ngazi za juu kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia shambulizi hilo lililoishtua Israel pamoja na jamii ya kimataifa, na kwenye barua ya kujiuzulu, Haliva amekiri hilo.

Taarifa ya jeshi la Israel - IDF - imesema, imeafikiwa kwamba Meja Jenerali Haliva atahitimisha majukumu yake na kustaafu jeshi, baada ya mrithi wake kuteuliwa katika utaratibu wa kitaalamu.

Wanamgambo wa Hamas walifanya shambulizi kubwa kabisa nchini Israel mnamo Oktoba 7, mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 1,170 na hasa raia, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP, zikinukuu mamlaka za Israel.

Tangu wakati huo, Israel imeapa kuliangamiza kundi la Hamas na kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo linalotawala Ukanda wa Gaza.

DW