Mwigulu awaita w’biashara kuwekeza Kanda ya Ziwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:01 AM Sep 19 2024
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba
Picha:Vitus Audax
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara Kanda ya Ziwa kuchangamkia fursa za kibiashara katika Soko Kuu la Kisasa la Mwanza, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 96.

Alitoa wito huo juzi jijini hapa baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, ambako alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kusema utekelezaji wake umezingatia viwango vya kimataifa na matakwa ya kimkataba.

“Mkataba uliopo baina ya wananchi na serikali ni kuhakikisha tunawaletea maendeleo kwa kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambavyo ndicho kitu tunachokifanya kwa sasa, hivyo wajiandae tu kuanza kupata matunda ya mradi huu muhimu katika uchumi wa Kanda ya Ziwa,” alisema.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Erick Mvathi alisema umefikia asilimia 96 na zaidi ya Sh. bilioni 21 zimelipwa kwa mkandarasi pamoja na fedha za madai ya utekelezaji kwa wakati.

Alisema soko hilo kwa ujumla linatarajiwa kutumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 1,400, huku kilichosalia ni pamoja na sehemu ya kuhifadhia taka, kupaka rangi, utengenezaji wa mifumo ya maji pamoja na mifumo ya umeme.

Aidha, alisema soko hilo lina maduka makubwa na madogo 514, vizimba 332, maeneo ya kuuzia samaki 372, vizimba vya machinga 167 pamoja na eneo la kuegesha magari 192.

“Likikamilika soko hili pekee tunatarajia kukusanya zaidi ya Sh.bilioni 3.7 kwa mwaka na pia utekelezaji wake umetoa ajira kwa vijana 175 ambao pia wanaendelea na utekelezaji wake,” alisema Mvathi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, alisema wamepokea zaidi ya Sh.bilioni 350 ambako Sh.bilioni 111 ni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu.

Alisema Sh.bilioni 23 ni kwa ajili ya soko kuu, stendi kuu ambayo imegharimu Sh.bilioni 17 pamoja na utekelezaji wa miradi ya barabara Sh. bilioni 11.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuwela mawe ya msigi pamoja na kufanya mikutano ya hadhara.

Miradi huo unatekelezwa na mkandarasi Mohamed Builders kwa Sh. bilioni 23.3 pamoja mkandarasi mshauri OGM Consultant ambaye analipwa Sh.bilioni 2.8 ulianza kutekelezwa Septemba 30, mwaka 2019.

Hata hivyo, ujenzi wake ulisimama kutokana na sababu za kifedha, hali ya kijiografia pamoja na usambazaji wa vifaa uliokwamishwa na janga la ugonjwa wa corona, ulitarajia kukamilika Aprili, 2022.

Inaelezwa kuwa kutokana na changamoto ya malipo kwa mkandarasi mradi huo haukukamilika kwa wakati, hivyo mkandarasi kuomba kuongezewa muda hadi Machi 25, mwaka huu.