Madiwani walia na tembo wavamizi

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:35 AM May 04 2024
Tembo.
Picha: Maktaba
Tembo.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Itigi mkoani Singida, limeiomba serikali kuwahamisha tembo ambao wako karibu na makazi ya watu kabla ujenzi wa tuta la mradi wa reli ya kisasa (SGR) haujakamilika ili iwe rahisi kuwarejesha kwenye Hifadhi ya Rungwa.

Wakitoa ombi hilo juzi kwenye kikao cha baraza hilo, walisema tembo wamekuwa kero kubwa hususani katika kata za Mgandu, Sanjaranda na Kitaraja na wanaharibu mazao mashambani na kusababisha vifo vya watu mara kwa mara. 

Diwani wa Mgandu, Richard Kapona, alisema tuta hilo litakapojengwa kabla ya kuwahamisha tembo hao kwenye makazi ya watu kutakuwa na uzio hivyo hakutakuwa na mapito hali itakayoleta ugumu kuwahamisha.

Naye Ofisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Tanzania (TAWA) Kanda ya Kati, Winnie Kweka, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikichukua hatua ya kuwahamisha tembo hao kutoka kwenye makazi ya watu kwa kutumia mabomu ya pilipili.

Alisema mabomu hayo yanatengenezwa kwa kutumia mchanga ambao unachanganywa na pilipili iliyosagwa na kuwekwa kwenye mpira na kilipuzi ambacho kinakuwa na utambi ambalo hurushwa walipo tembo hao na kulipuka.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Hussein Simba, alisema serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa za kuwaondoa tembo kutoka kwenye makazi ya watu na kuwasaidia wale wanaopata tatizo la mazao yao kuharibiwa ba tembo hao.

Mwaka juzi, Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Tanzania (TAWIRI) ilitoa elimu na mafunzo ya utatuzi wa migongano baina ya wanyapori na binadamu kwa kutumia mbinu rafiki za kudhibiti wanyama waharibifu kwa wananchi wa halmashauri ya Itigi.

Taasisi hiyo ilitoa mafunzo hayo kwa wakulima 30 kutoka kata za  Mwamagembe, Sanjaranda, Itigi, Majengo na Kitaraka.

Timu hiyo ya wataalamu kutoka TAWIRI iliongozwa na Dk. Janemary Ntalwila, na iliwafundisha wananchi baadhi ya mbinu za kuwadhibiti tembo ikiwa ni pamoja na vitisho vya mwanga,vitisho vya sauti (vuvuzela au honi kali),mabomu ya pilipili, matumizi ya fataki,uzio wa vitambaa vyenye mafuta ya oili na pilipili,Tofali la pilipili na matumizi ya fensi ya mizinga ya nyuki.

 Aidha, walifundishwa njia mbadala ya upandaji wa mazao kinga katika maeneo yanayoathirika na tembo kuwa ni njia nzuri ya kupunguza migongano .

 Baadhi ya mazao hayo ni pamoja na tumbaku, pilipili, ufuta na tangawizi ambayo yanaweza kupandwa kuzunguka shamba au kama mazao mbadala.

 Njia hizo zimethibitika katika maeneo mengi kuwa na matokeo chanya ya kupunguza uvamizi na uharibifu wa mazao na madhara mengine yanayotokana na uvamizi wa wanyamapori hao waharibifu.