HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imefanya vizuri kwa kuwa na kasi ya ukusanyaji wa mapato na uratibu mzuri wa fedha.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati wa ziara yake ya siku tatu aliyoifanya katika Wilaya ya Ilala wakati wa kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
RC Chalamila ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika kituo cha Afya cha Kinyerezi na kubainisha alitoa ofa ya Halmashauri itakayofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ataipa ofa ya kuwaongezea miradi.
Amebainisha tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali kwa jiji hilo kuwapa Bilion 21 kwaajili ya ujenzi wa hospitali tatu katika kila jimbo katika Wilaya ya Ilala na kila moja itagharimu kiasi cha Shilingi Bilion 7.
Hivyo tayari Billion 15 zimeshahamishwa na kila kituo itaingiziwa Billion 5 kwa ajili ya kuanza kwa mradi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza katika ziara hiyo akiwa katika kituo cha Afya Kinyerezi na mkutano wa hadhara ulifanyika Kimanga amewataka wananchi waendelee kuwa wavumilivu na ustahimilivu kwani Serikali ya Tanzania ni sikivu na itaenda kutatua changamoto zote zinazowakabili wananchi.
DC Mpogolo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaingizia fedha nyingi Wilayani humo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo na kutatua kero za wananchi ambapo shule mpya za ghorofa zinaendelea kujengwa, vituo vya afya na barabara kujegwa kwa kasi kubwa.
Pia aliweza kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kwa kutembelea majimbo yote matatu Ukonga, Segerea na Ilala kwani ziara yake imekuwa na mafanikio makubwa na inaonyesha jinsi gani Serikali ni sikivu kutatua shida za wananchi na kuboresha huduma za kijamii.
“Nikuhakikishie Mkuu wa Mkoa tutaenda kusimamia haki, kusimamia miradi yote na kusimamia mapato ipasavyo na tutaenda kusimamia uchaguzi wa haki na ustawi na hakutakuwa na mtu ambae atamtisha mwenzio kwa namna yoyote ile kipindi cha uchaguzi” amesema Mpogolo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Mrisho Satura amesema Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam inajikita katika kutatua na kuleta maendeleo kwa wananchi wake na kutelekeza maagizo na sera kuwafikia na kubadilisha dira kwa wananchi wake.
Amefafanua tayari barabara ya Kimanga- Mazda itaanza kujengwa upya kwa ngazi ya rami na kwenda kumaliza kero inayowakabili watumiaji wa barabara hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo katika kata ya Gerezani barabara ya mtaa Lindi ambayo ni kero kwa watumiaji na wenye vyombo vya moto amewatoa hofu wafanyabiashara na madereva hakuna mapato yanayopotea kwa ushuru wa Sh.2000 wanayopotea kwa siku kwani ushuru huo wanauatambua.
Amefafanua kwa kipindi cha mwezi mmoja wa mwezi Aprili wamekusanya mapato ya Sh. Mil.18 kutokana na ushuru huo.
Amesema kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na jiji hilo tayari wameibuka kidedea kwa ukusanyaji mzuri wa mapato na kuahidi kulibadilisha hadhi jiji la Dar es Salaam kwa kuijenga upya kwa kutekeleza miradi mikubwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED