DC awapa mbinu wadau wa alizeti kuwa mabilionea

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 12:43 PM Sep 18 2024
Zao la alizeti
Picha:Mtandao
Zao la alizeti

MKUU wa Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, Emmanuela Kaganda, amewataka wakulima wa alizeti na wafanyabiashara ya mafuta ya kula, kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa ili kutengeneza mabilionea wa zao hilo.

Alisema kufunguka kwa Soko la Eneo Huru la Afrika (AfCFTA), ambalo linakadiriwa kuwa na walaji zaidi ya bilioni 1.3 kutoka nchi 53 Afrika ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Kaganda alikuwa akizungumza juzi na wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wakati wa hafla ya utiaji  saini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa zao la alizeti.

Mkataba huo ulihusisha kati ya Taasisi ya Maendeleo ya Afrika ya US African Development Foundation (USADF) na Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko cha Mbungwe.

“Ni muhimu sana tukaweka jitihada za dhati kuyafikia masoko haya na siyo kuwa waangaliaji tu na kulalamika. Niwaombe sana wataalamu wa serikali, kuwasimamia wakulima.

“Na katika mradi huu, niwahakikishie USADF, kwamba Mbugwe AMCOS itafanya vizuri na kupata Dola za Marekani 250,000. Kupitia mradi huu pia, matumaini ya serikali ni kuanzisha viwanda na kutengeneza mabilionea.”

Mkoa wa Manyara ni kati ya mikoa nchini inayolima alizeti lakini tija ni ndogo kutokana na wakulima wengi kutumia mbegu za kienyeji ambazo hazijafanyiwa utafiti.

Watafiti na wahaulishaji wa teknolojia za kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),  wamekuwa wakieleza katika machapisho mbalimbali nchini kuwa, hivi sasa  mbegu ya ‘record’ na mbegu nyingine mpya zilizofanyiwa utafiti, ambazo zimetambulishwa kwa wakulima waanze kuzitumia, kwa kuwa zina tija kubwa.

TARI inahamasisha matumizi ya mbegu hizo, kwa sababu zinastahimili mabadiliko ya tabianchi na bei ya wastani ambayo wakulima wengi wanamudu kununua, lakini pia zina tija katika uzalishaji.

Katika hafla hiyo, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Manyara, Absalum Cheliga, alisema mradi huo umekuja kuwanyanyua kiuchumi wana ushirika na unagusa uzalishaji na masoko.

Kwa upande wake, Ramadhan Mangi, alisema Mbugwe AMCOS, itaongeza thamani na wakulima, watapata fedha nyingi hivyo aliwashauri wafanye kazi kwa bidii na kulima kwa wakati na kupanda kwa wakati ili wapate mazao mengi.