Bashe atishia kumtumbua Mrajisi Vyama vya Ushirika

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:21 AM Apr 18 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, amemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege kumaliza suala la ubadhirifu kwenye vyama vinginevyo nafasi yake itakuwa matatani.

Alimpa agizo hilo jana jijini hapa alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 14 wa wadau wa kahawa nchini.

Bashe alisema suala la wizi katika vyama vya ushirika nchini linapaswa kukomeshwa mara moja kwani limekuwa moja ya sababu ya kuwanyonya wakulima.

"Kuna vyama vya ushirika viongozi wake wamechukua Sh.milioni 200 za wanunuzi wa kahawa lakini wamegoma kurejesha fedha hizo wala kutoa kahawa na deni hilo lote linabebwa na wakulima.

"Nakuagiza wizi huu na ujambazi unaofanywa katika vyama hivi unakwisha mara moja na mimi Ma DG wengi wa wizara hii ambao nimewaondoa kwenye nafasi zao ni kwasababu nilikua nawaambia kama hivi lakini hawachukui hatua"alisema Bashe

Alisema, viongozi wote ambao wamehusika kwenye wizi ndani ya vyama vya ushirika wanapswa kufikishwa mahakamani kwa kosa la wizi na siyo madai kama ilivyo sasa. 

Aidha, alisema vyama vingi vya ushirika licha ya viongozi wake kuwa wezi lakini vimekuwa ni sehemu ya kunyonya wakulima kwa kuweka tozo nyingi. 

Kadhalika, Bashe aliwata viongozi wa vyama vya ushirika kuandaa mahitaji ya wakulima na kuyawasilisha Bodi ya Kahawa ili yafanyiwe kazi. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa, Prof. Aurelia Kamuzora, alisema malengo ni kuzalisha tani 300,000 za kahawa ifikapo mwaka 2025 kutoka tani 80 za hivi sasa.

Pia, aliwataka wakulima wa kahawa nchini kutumia mfumo rasmi wa uuzaji zao hilo na kujiepusha na walanguzi ambao wamekuwa wakiwadanganya kuuza kwa bei ya hasara.

 Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile, alisema wataendelea kuisimamia serikali kutenga bajeti ya kutosha katika sekta ya kilimo.

Ditopile alisema ipo haja ya kuwekeza katika soko la ndani ili kuwa na uhakika kwa wakulima tofauti na ilivyo sasa ambapo kiasi kinachouzwa nje kinaongezwa thamani na kurudi nchini kwa bei ya juu.