Bajeti TARURA Dodoma yafikia bil. 66.2/-

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:56 AM May 09 2024
Meneja Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo,
Picha: Paul Mabeja
Meneja Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo,

KATIKA kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, bajeti ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja kwa mkoa wa Dodoma imeongezeka kutoka Sh. bilioni 12.7 mwaka 2020/21 hadi Sh. bilioni 66. 2.

Meneja Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo, alibainisha hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ofisi yake katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.

Mhandisi Lemelo alisema ongezeko hilo la bajeti ni kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2023/24 ambalo limeongezeka kwa asilimia 412.77 tangu Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021.

Pia alisema ongezeko la bajeti hiyo limesaidia kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara za lami na zege kutoka kilomita 171.29 hadi 309.71 katika kipindi hicho. 

“Barabara za changalawe zimeongezeka kutoka kilomita 1,258.65 mwaka 2020/21 hadi kilomita 1,827.5 mwaka 2023/24. Pia madaraja 19, maboksi kalavati 45 na mifereji/mitaro yenye urefu wa mita 73,822.24 vimejengwa.

“Aidha, taa za barabarani 470 zimesimikwa, barabara mpya zenye urefu wa kilomita 544.60 zimefunguliwa ambazo hazikuwapo kabisa, hii inaakisi kaulimbiu yetu ya tunakufungulia barabara kufika kusiko fikika,” alisema Mhandisi Lemelo.

Kadhalika, alisema mtandao wa barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka asilimia 10, Februari 2021 hadi kufikia asilimia 34.70 Machi 2024.

Alisema, barabara zenye hali mbaya zimepungua kutoka asilimia 60 Februari 2021 hadi asilimia 31 Machi 2024.

Vile vile, alisema katika kipindi hicho cha miaka mitatu, TARURA mkoa wa Dodoma imeongeza vitendea kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.

“Magari manane mapya yamenunuliwa na kusambazwa katika ofisi za mameneja wa wilaya na mkoa, ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa barabara ikiwamo ‘Motor Grader’, ‘Roller’, ‘Bulldozer’ na ‘Excuvator’ na ‘Loadbed’ vimenunuliwa na kukabidhiwa kwa meneja wa Wilaya ya Chamwino. Ununuzi  wa vitendea kazi umerahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa kazi za wakala,” alisisitiza.

Meneja huyo pia  alisema idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 69 mwaka 2021 hadi 84 mwaka 2024 wakiwamo wa kada ambazo awali hazikuwapo ambazo ni mkaguzi wa ndani, mchumi na ofisa maendeleo ya jamii.

Pia alisema TARURA mkoa imeendelea kutekeleza miradi ya kielelezo ikiwamo ujenzi wa barabara za lami katika mji wa serikali za kilomita 12.6, ujenzi wa barabara ya lami Mwanga - Kisasa – Medelii kilomita 10.7 na barabara ya lami Swaswa – Mpamaa – Arusha Road Jct kilomita 8.2.

Mingine ni ujenzi wa barabara ya lami ya mzunguko Mlimwa kilomita 1.55, barabara katika Soko la Machinga kilomita 0.6 na barabara ya kuzunguka Makazi ya Waziri Mkuu kilomita mbili.