Vijana hawa wanatoa wapi ujasiri huu?

By Joseph kulangwa , Nipashe Jumapili
Published at 03:19 PM Apr 28 2024
Wanafunzi kidato cha kwanza.
PICHA: MAKTABA
Wanafunzi kidato cha kwanza.

ZAMANI tulipokuwa tukijiunga na kidato cha kwanza baada ya kufaulu darasa la saba na si kuchaguliwa kama inavyosemekana leo, tulitangulia kwenda shuleni kabla wenyeji hawajawasili.

Sisi tukiitwa ‘njuka (new comers)’ au ‘wapya’, tuliwahishwa ili kuzoea mazingira kabla wale wa kidato cha pili na kuendelea, hawajaripoti kutoka likizo ya mwaka ili kuanza mwaka mpya na kidato kipya.

Na walipofungua wenyeji kama wiki mbili baadaye, wale wa kidato cha pili walikuwa na shughuli nasi. Walitutesa kwa kile walichokuwa wakidai ni kututoa ugeni.

Sitaki kukumbushia hali ilivyokuwa enzi hizo bali itoshe tu kusema tulipitia ya kupitia, nasi kufanya hivyo tulipokuwa kidato cha pili tukilipiza kisasi kwa wasio na hatia. Lakini ndio ulikuwa utaratibu ingawa si rasmi. Niliripoti kidato cha kwanza katika sekondari iliyokuwa ya wavulana watupu ikiwa jirani na sekondari ya wasichana watupu lakini zote zikiwa na jina linalofanana huku ‘Boys’ na kule ‘Girls’.

Hata hivyo, nilikuwa na rafiki aliyeniacha shule ya msingi huku yeye akichaguliwa kujiunga nA sekondari hiyo, akiwa amenitangulia miaka. Nilifarijika kuwa na ‘skulumeti’, hivyo nikiamini nisingepitia mateso ya jamaa wa kidato cha pili.

Ingawa hiyo haikuzuia, sikula suluba kama walivyokula wenzangu kwa sababu jamaa yangu alikuwa mbabe fulani hivi, hivyo akanifanya kuwa ‘lokaboi (lockerboy)’ wake.

Lokaboi alikuwa kijana wa kidato cha kwanza aliyemhudumia wa kidato cha tatu, kumfuatia chakula bwaloni na kumwoshea vyombo na ilizoeleka yakawa maisha ya kawaida kwani lokaboi kuna nyakati alinufaika na huduma hiyo kwa chakula cha ziada.

Lakini kabla hatujaanza masomo rasmi, siku chache baada ya wenyeji kuwasili, siku moja jamaa yangu akanitaka nijianadae ili tutoke pamoja jioni, bila hata kuniambia safari ilikuwa ya wapi. Mimi nani nikatae!

Kwa kumwamini nilimwacha nje akiwa na wenzake, nikaingia bwenini kubadili nguo tayari kwa safari hiyo isiyojulikana mwelekeo wake. Nilikawia bwenini kiasi fulani na nilipotoka, sikumkuta na hata wenzake sikuwaona.

Kwa kuwa sikujua mweleko wa safari, nilirudi bwenini kubadili nguo na kuvaa za kawaida zisizo na uhusiano na safari, nikajifanyia mambo mengine jioni hiyo ikiwa ni pamoja na kujiandaa kumchukulia chakula.

Lakini kabla muda wa chakula haujawadia, zikasambaa taarifa shuleni kuwa kuna wanafunzi kutoka ‘Boys’ wamekwenda ‘Girls’ na kushambulia walimu waliokuwa wakiwazuia kuonana na wasichana!

Kweli, ghafla tukasikia kengele ikigongwa muda usio wake, tukajua lazima kuna dharura. sote tukatoka tulikokuwa na kwenda mstarini, tukakuta mwalimu wa zamu na wengine wakiwa wamehamanika.

Tulipotulizana msitarini, ndipo mwalimu wa zamu akatutangazia kuwa kuna wenzetu wamevamia shule ya wasichana na kushambulia walimu, hivyo uongozi umeamua kuwasimamisha masomo mpaka wizara itakapoamua vinginevyo.

Enzi hizo, uongozi wa shule haukuwa na mamlaka ya kufukuza mwanafunzi mpaka kesi ifike wizarani na ikijiridhisha, ndipo hatua zichukuliwe kulingana na uzito wa kosa. Bahati mbaya sana jamaa yangu alikuwa mmojawapo. Walifukuzwa hatimaye.

Sikushituka sana kusikia uhusika wake lakini nilijifikiria kuwa endapo nami ningekuwa kwenye msafara huo, ningekuwa mgeni wa nani kwenye familia yetu kwamba hata masomo ya kidato cha kwanza sijaanza nimetimuliwa! Nilimshukuru Mungu kwa kunichelewesha bwenini siku hiyo.

Kesho yake, Mkuu wa Shule akatutangazia rasmi uamuzi ule na kusema si rahisi shule kuvumilia kuishi na wanafunzi wa tabia kama ile wasioogopa kutoroka shule na kwenda shule nyingine tena ya wasichana, kufanya fujo ikiwa ni pamoja na kushambulia walimu.

Nimekumbuka tukio hili, kutokana na kauli zinazotolewa siku hizi na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) bila hofu dhidi ya watu wengine wakiwamo wapinzani na hata viongozi wa juu wa serikali na CCM!

Nakumbuka tukio la kijana mmoja kuwasema viongozi wastaafu wa kitaifa eti wanaweweseka... eti wakae kimya kutokana na zama zao kupita, wasiharibu nchi na kumpotezea mwelekeo Mkuu wa Nchi na kwamba wakizidi watatwangwa!

Mwingine akaunganisha akisema badala ya kunyamazisha wapinzani kwa risasi watatumia sindano, huku akisisitiza kuwa serikali ya CCM haiwezi kupeleka maendeleo kwenye majimbo yanayoshikiliwa na wapinzani! Hata mwingine akamtishia maisha kiongozi wa upinzani kuwa angemmaliza.

Hivi karibuni, akaibuka mwingine akawaambia polisi wasijishughulishe kutafuta watu watakaopotezwa kwa kutukana viongozi. Maana yake ni kwamba watakuwa wameshauawa, hivyo polisi wafanye mengine na si kutafuta wendazao!

Hawa wana tofauti gani na wale jamaa zangu waliotoroka shule kwenda kufanya fujo shule nyingine tena ya wasichana, bila hata kutaka kuheshimu nafasi na hadhi za walimu wao? Leo tunashuhudia wapo wakidunda, wakibadilisha vituo vya kazi kama nguo. Mungu tuhurumie tu!