Haaland asaini mkataba mrefu Man City

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:37 AM Jan 19 2025
ERLING Haaland.
Picha: Mtandao
ERLING Haaland.

ERLING Haaland ametia saini mkataba mpya uliovunja rekodi wa miaka tisa na nusu katika klabu ya Manchester City, klabu hiyo imetangaza.

Mshambuliaji huyo alikuwa chini ya mkataba hapo Etihad hadi 2027, lakini ameongeza mkataba wake hadi 2034.

Kiwango halisi hakijawekwa wazi na City, lakini vyanzo vimeiambia ESPN kwamba ni kati ya mikataba yenye faida kubwa katika historia ya klabu hiyo.

Mkataba mpya wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 pia umeondoa vipengele vya ununuzi ambavyo vilijumuishwa katika mkataba wake alipowasili kutoka Borussia Dortmund mwaka 2022.

Mkataba wa miaka tisa na nusu ndio mrefu zaidi kusainiwa na mchezaji katika historia ya Ligi Kuu England, ukipita mkataba wa miaka tisa wa Cole Palmer aliosaini na Chelsea mnamo Agosti 2024.

Haaland amekuwa akihusishwa kuhamia Hispania katika siku zijazo, huku Real Madrid na Barcelona zikionesha nia siku za nyuma.Hata hivyo, mkataba mpya wa raia huyo wa Norway sasa unatazamiwa kumuweka Man City baada ya kutimiza miaka 33.

"Nina furaha sana kusaini mkataba wangu mpya na kuweza kutazamia kutumia muda zaidi katika klabu hii alisema Haaland.

"Manchester City ni klabu maalum, iliyojaa watu wa aina yake na ni aina ya mazingira ambayo husaidia kuleta ubora kutoka kwa kila mtu.

"Pia nataka kumshukuru Pep Guardiola, wasaidizi wake, wachezaji wenzangu na kila mtu katika klabu kwani wote wamenisaidia sana katika miaka michache hii. Wameifanya hapa kuwa mahali maalum. Sasa nataka kuendelea kujiendeleza, kuendelea kufanya kazi ili kuwa bora zaidi n kupata mafanikio zaidi mbeleni."