Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, ametoa hoja katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais Samia Suluhu Hassan awe mgombea wa nafasi ya urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Vilevile, Kimbisa amependekeza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, naye awe mgombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo.
Hoja hiyo, iliyowasilishwa leo Jumapili, Januari 19, 2025, katika kikao kinachoongozwa na Rais Samia jijini Dodoma, imeungwa mkono kwa shangwe na wajumbe wote wa mkutano huo, ambao walisimama kuonyesha ridhaa yao.
Wajumbe wa mkutano huo wamesema pendekezo hilo linatokana na ubora na ufanisi wa viongozi hao katika kutekeleza Ilani ya CCM ya 2020/2025.
Wakichangia taarifa za utekelezaji wa ilani hiyo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, wachangiaji wamesisitiza kuwa hakuna mbadala kwa Rais Samia na Dk. Mwinyi kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata katika kuendesha Serikali na chama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED