RIPOTI MAALUM- 2 Sababu kukithiri utapishaji vyoo milimani jijini Mwanza

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 10:43 AM Jan 19 2025
Sababu kukithiri utapishaji  vyoo milimani jijini Mwanza.
Picha: Vitus Audax
Sababu kukithiri utapishaji vyoo milimani jijini Mwanza.

KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii, ilielezwa utiririshaji wa vinyesi kwa watu waishio milimani nyakati za mvua unavyohatarisha maisha ya wakazi wa Jiji la Mwanza. Sehemu hii ya pili, inabainisha sababu hasa zinazofanya hali hiyo iendelee Jiji la Mwanza...

LICHA ya tatizo la utiririshaji majitaka kutoka katika vyoo vya watu waishio milimani kwenda katika makazi ya watu kuendelea kuwakabili wakazi wa Jiji la Mwanza, sababu kubwa imebainika kuhusu kuendelea kuwapo kwa hali hiyo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira wa Jiji la Mwanza, Desderius Polle, anasema jiji hilo lenye watu 426,154 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inalo gari moja pekee kwa ajili ya utapishaji vyoo katika makazi ya watu.

Pia anasema jiji hilo linategemea pia magari mengine kutoka  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) yenye jukumu la udhibiti wa majitaka pamoja na wadau wengine ambao wamechukua tenda kushughulikia majitaka.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004, Kifungu cha 123 cha Usimamizi wa taka Vimiminika, inazitaka mamlaka za serikali za mitaa kushughulikia na kuondoa taka vimiminika toka majumbani na maeneo ya biashara. 

Kadhalika, Sera ya Afya ya mwaka 2007, kipengele  cha 5.3 (1) kuhusu udhibiti wa magonjwa, inaitaka serikali kulinda afya za wananchi kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya stadi za maisha na afya ya mazingira.

Hata hivyo, uondoshwaji majitaka kwa wakazi wa milimani jijini Mwanza hausimamiwi ipasavyo hali inayosababisha utapishaji vyoo usio salama pamoja na utengenezaji wa chemba za kutegesha zinazotiririsha taka kwenda  katika makazi ya watu na vyanzo vya maji likiwamo Ziwa Victoria nyakati za mvua

Ofisa Afya Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo, anasema ziko jitihada za kudhibiti. Anasema mbali na halmashauri kuwa na gari moja la kunyonya majitaka, bado yako magari mengine saba yanayotumiwa na wadau wenye tenda pamoja na MWAUWASA ambayo yanafanya kazi ya kunyonya majitaka katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na mfumo wa moja kwa moja.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004 kifungu cha 187(1) kinamweka hatiani mtu yeyote ambaye atamwaga vitu vyovyote vya hatari, mafuta, michanganyiko ya mafuta kwenye ardhi, maji, hewa au mazingira oevu. Adhabu  ya kosa hilo ni faini isiyopungua Sh. milioni tatu na isiyozidi Sh. milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka 12 jela au vyote viwili.

Pia kifungu kidogo cha (2) kinaeleza kuwa pamoja na adhabu yoyote ambayo Mahakama inaweza kutoa kwa mtu aliyetiwa hatiani kwa kukiuka masharti ya kifungu cha (1), pia inaweza kumwamuru mtu huyo kulipa gharama zote za kusafisha mazingira yaliyochafuliwa na kuondoa uchafu. 

1

WANAIJUA SHERIA?

Baadhi ya Wakazi wa maeneo ya milimani wanasema sheria hizo hawazifahamu na kuwa wengi wao wamekuwa wakifanya hivyo kwa uficho wakikwepa gharama za kutapisha.

Mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa, Mariam Husein, anasema umekuwa utaratibu wa kawaida kwa wakazi wa maeneo ya juu kutiririsha kinyesi na kuwa wakati wa mvua amekuwa akishuhudia uchafu huo katika mitaro.

Hata hivyo anasema uwezo kwa baadhi ya wananchi waishio katika maeneo hayo ni duni, hivyo wanakimbilia njia hiyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kugharamia magari ya kunyonya majitaka.

“Wanafanya hivyo kwa kuwa hawana elimu sahihi. Hali  hii inatishia afya zetu na watoto kwani mvua ikinyesha tunalazimika kuwazuia watoto wasitoke nje kwani ndio waathirika wakubwa wa tatizo hilo,” anasema.

Abdul Khasim, Mkazi wa Kirumba, anasema ziko sababu mbalimbali za utiririshaji ikiwamo kukwepa gharama za utapishaji na maeneo kutokufikiwa na magari ya utapishaji hasa milimani.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira wa Jiji la Mwanza, Desderius Polle, gharama za utapishaji vyoo zinategemea umbali wa eneo husika lakini hazizidi Sh. 120,000.

Kuhusu tatizo la ufikiwaji wa wananchi wa milimani, Polle anasema miundombinu barabara si rafiki kwa makazi ya milimani kutokana na ujenzi kwenye maeneo hayo kutokuruhusu upitishwaji wa magari hayo.

Mkazi wa Mabatini, Juliana Elias, anasema sababu kubwa inatokana na tatizo la maeneo husika ya milimani kutokuruhusu ujenzi wa choo cha kina kirefu hali inayowalazimu kujenga vyoo vya muda mfupi, hivyo kutumia utaratibu huo kuondosha kinyesi kwenye chemba zao.

Nelson Joseph, Mkazi wa Kilimahewa, anasema mfumo huo umezoeleka kwa jina la kufungulia koki na umekuwa ukitumika mara kwa mara.

Joseph anasema sababu ya kufungulia chemba hizo ni pamoja na maeneo wanayoishi kutokuwa rafiki kwa kuchimba choo kirefu maeneo yenye miamba hivyo kutengeneza shimo fupi wakitegemea mvua inyeshe.

Mkazi wa Ghana Aman Kyasekile anasema tatizo la uelewa na kutokuchukuliwa hatua kali imekuwa sababu ya ufunguliaji wa chemba hizo kwa watu waishio milimani na kuwa wanatumia kigezo hicho ili kurahisisha kuondosha uchafu wao.

“Kujaa kwa chemba ndiyo sababu ya kuruhusu ili yaende na maji na hii imekuwa ikisababisha uchafuzi wa mazingira pamoja na kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko,” anasema Kyasekile.

Takwimu za kaya zenye vyoo bora katika Kata ya Igogo ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kwa kuwa na wagonjwa wa kipindupindu hivi karibuni, zinaonesha asilimia 83.68 hazina vyoo bora.

Kati ya kaya 7439 katika kata hiyo,  ni Kaya 1214 pekee zenye vyoo bora sawa na asilimia 16.3 huku zaidi ya 6220 sawa na asilimia 83.68, zikiwa hazina  hali inayohatarisha zaidi maisha ya wakazi hasa wakati wa mvua. 

SHERIA YA MAZINGIRA

Licha ya sheria ya mazingira kuipa jukumu serikali za mitaa juu ya usimamizi na udhibiti wa uchafuzi wa taka vimiminika, Sheria Namba 5 Ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 Sura ya Nne, Kifungu namba 21 (h) inaziruhusu Mamlaka za Maji kuingia katika makubaliano ya biashara ya taka kwa ajili ya utupaji wa taka kwenye mfumo wa maji taka.

Kadhalika kifungu namba 31(a) kimezipa mamlaka hizo leseni ya kujenga na kutunza mabomba makuu ya usambazaji maji na pale inapohitajika kulingana na leseni yake, mifumo ya maji taka.

Kutokana na jukumu hilo, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa MWAUWASA,  Mhandisi Salim Lossindilo, anasema ufinyu wa bajeti ndilo tatizo la kuzifikishia kaya mfumo wa maji taka wa ‘simplified sewerage system’.

Anasema tayari walishaanza utekelezaji wa mradi wa kuondosha majitaka kwa mfumo huo katika baadhi ya maeneo kupitia mradi uliolenga kuunganisha kaya 1,000 na kuishia kuunganisha kaya 300 pekee kutokana na ufinyu wa bajeti.

“Kwa maeneo ambayo yaliunganishiwa yamekuwa na matokeo mazuri kwani maeneo hayo yalikuwa pia na tatizo kubwa la utiririshaji majitaka ovyo kwasasa hakuna huo utiririshaji wa maji taka,”anasema Mhandisi Lossindilo.

Pia anasema usimikaji wa miundombinu hiyo ni ghali hivyo siyo rahisi kumtupia mzigo huo mwananchi bali kinachofanyika kwa sasa ni kutafuta wadau ambao watawekeza katika kusimika na kusaidia miundombinu hiyo kuwafikia wananchi ili wao wachangie gharama za kutibu na marekebisho.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za MWAUWASA hivi karibuni katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka  2024/25, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Neli Msuya, alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, kaya 6,245 ziliunganishwa kwa mkoa mzima wenye zaidi ya watu milioni tatu.

Alisema huduma hiyo ya uondoshaji majitaka ina mtandao wa mabomba yenye urefu wa kilometa 149.27 pamoja na mabwawa 17 ya kutibu taka hizo yaliyoko katika eneo la Butuja/Sabasaba wilayani Ilemela.

“Kutokana na jiografia ya jiji la Mwanza kuwa ya miinuko, majitaka husafirishwa kwa kusukumwa kwa pampu ambazo ziko katika vituo vya Makongoro, Mwaloni-Kirumba na Mwanza Kusini-Igogo,” alisema Msuya.

Itaendelea…….