MATOB0 YA BAJETI: ACT yasema bajeti haijibu changamoto za wananchi

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 07:56 AM Jun 23 2024
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu,  akizungumza wakati wa mkutano wa uchambuzi wa bajeti ya serikali mwaka 2024/25, Dar es Salaam jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, akizungumza wakati wa mkutano wa uchambuzi wa bajeti ya serikali mwaka 2024/25, Dar es Salaam jana.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema bajeti ya serikali inayopendekezwa kwa mwaka ujao wa fedha, haijibu changamoto sugu zinazokabili wananchi na ipo kimatabaka.

Hayo yalisemwa jana mkoani Dar es Salaam na Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchambuzi wa bajeti inayopendekezwa uliofanywa na chama hicho.

Alisema bajeti ya serikali inayopendekezwa haijagusa kikamilifu kilio cha kikokotoo kwa wastaafu licha ya serikali kupendekeza kuongeza kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa kundi la watumishi wa umma walio chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) huku kundi la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Taifa (NSSF) likiwa na pendekezo la kuongezwa kutoka asilimia 33 hadi asilimia 35.

Alisisitiza kwamba kilio cha wastaafu wengi kinaitaka serikali irejeshe kikokotoo cha mafao cha awali cha asilimia 50 ya mafao ya mkupuo na hivyo wengi hawajafurahia ongezeko hilo.

Alisema bajeti pendekezwa pia haijagusa maisha ya Watanzania kwa kuwa walio wengi wako katika maisha magumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kutokana na kodi na tozo.

"Bajeti haijibu changamoto za Watanzania, kila inapotangazwa bajeti inakuwa si ya kuwaletea wananchi unafuu wa maisha, bajeti iliyowasilishwa bungeni inaonekana imejikita zaidi katika kulipa madeni na posho za viongozi serikalini kuliko kuboresha maisha ya Watanzania maskini kwa kuwaboreshea barabara, umeme, maji na sekta za afya na elimu," alisema Dorothy.

Kiongozi huyo alisema chama hicho kimeamua kuionesha serikali upungufu huo kwa maslahi mapana ya Watanzania ili kusaidia kupata bajeti itakayojibu changamoto za wananchi.

Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita alisema mapendekezo ya bajeti hiyo yamejikita katika kulipa madeni na posho za watawala na hayajagusa kikamilifu huduma bora za afya, elimu, nishati, mafuta na gesi asilia.

Pia alizitaja sababu ya serikali kushindwa kukusanya fedha na hatimaye kuangukia katika madeni na kuongeza tozo kuwa ni pamoja na rushwa, utoroshwaji mkubwa wa madini nchini, mikopo ya misaada ambayo serikali inakuwa haina uhakika wa kuipata na yenye masharti na riba kubwa, pamoja kukosa ubunifu wa kutawanya wigo wa vyanzo vya mapato.

"Tulijaribu pia kuangalia fedha za bajeti kwa mwaka 2O24/25 ni Sh. trilioni 49 zinakwenda wapi? Tukagundua mgawanyo wa matumizi unaonesha Sh.  trillion 34.6 imetengwa kwa ajili ya mshahara, posho, magari, misafara ya viongozi, chai ambayo ni sawa na asilimia 70 ya bajeti.

"Miradi ya barabara, mikopo ya wanafunzi, ujenzi wa madarasa, dawa, pembejeo za kilimo maji Imetengewa Sh. trilion 14.7 sawa na asilimia 30.

"Hii inaonesha Watanzania wenye kipato cha chini wanaendelea kuumia kwa kukosa huduma za msingi," alisema Mchinjita.  

Waziri Kivuli wa Fedha, Mipango na Hifadhi ya Jamii wa ACT Wazalendo, Kiza Mayeye alisema Deni la Taifa limeongozeka, hali aliyodai inahatarisha usalama wa nchi. 

Alisema mpaka Aprili mwaka huu, Deni la Taifa liliongezeka kutoka Sh. trilion 82.25 ya mwaka 2023 hadi kufikia kufikia Sh. trilion  91.7 sawa na ongezeko la Sh. trilion 12.6 (asilimia 15.9).

Alisema kuna jambo baya katika ukopaji nchini kwa kuwa fedha zilizokopwa zinaendesha miradi kwa hasara, akikumbushia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere inaonesha kuna ubadhirifu wa fedha zinazotokana na mikopo hiyo. 

Pia alishauri magari ya serikali yatumie gesi asilia badala ya kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi, akisisitiza hiyo itasaidia kupunguza gharama. 

"Bajeti ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukiisikiliza haijielekezi kutatua changamoto ya upungufu wa walimu, kila utakapokwenda utakuta shule haina walimu wa kutosha, kuna unafuu kwa shule za mijini, vijijini ndiko balaa, tatizo hili linazidi kukithiri kila mwaka. 

"Ukiiangalia bajeti ya serikali haijatenga fedha kwa ajili ya kuajiri walimu wengi, tuna vijana ambao wamemaliza vyuo hawana ajira, kila unapokwenda kwenye vijiji madarasa ni shida, watoto wanakaa chini, wazazi wanachangishwa fedha kujenga madarasa wakati hiyo ni kazi ya serikali," alisema. 

Hata hivyo, Ibara ya 8(1)(d) ya Katiba ya nchi inaeleza wananchi kushiriki shughuli za serikali yao. 

Waziri Kivuli huyo aliendelea: "Ukiangalia gharama za matibabu, mtu asiyekuwa na uwezo, kufa ni rahisi kwa sababu hana uhakika wa kupata matibabu bora. 

"Tumeona Watanzania wanapoteza maisha kwa kukosa fedha za kujihudumia katika zahanati zetu, unakuta kuna nesi mmoja au wawili bado, kuna changamoto ya huduma za afya." 

Vilevile alishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza viwanda vya kuzalisha sukari, ili kuondoka na uhaba wa bidhaa hiyo, akikumbushia kuwa mwishoni mwaka jana iliadimika mpaka kufikia kiwango cha kilo moja kuuzwa kwa Sh. 4,000 mpaka 5,000.