Shirikisheni wananchi miradi ya maendeleo

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:05 AM Oct 23 2024
 MWENGE wa Uhuru
Picha:Mtandao
MWENGE wa Uhuru

MWENGE wa Uhuru umehitimisha mbio za mwaka 2024 Oktoba 14 jijini Mwanza, kinachofuata ni maandalizi ya ratiba nyingine mwakani.

Katika kilele cha mbio hizo  wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, anasema miradi 16 yenye thamani ya Sh. bilioni 8.6 imekataliwa.
 
 Anasema tayari miradi hiyo imekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa hatua zaidi ili watakaohusika kuikwamisha, sheria ifuate mkondo wake.
 
 Hatua hiyo ni nzuri na inaweza kusaidia kukomesha vitendo vya hujuma kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekuwa ikihujumiwa kwa kutekelezwa chini ya kiwango.
 
 Umefika wakati sasa ushirikishaji wananchi kulinda miundombinu ya miradi ya maendeleo upewe kipaumbele ili nao wawe na mchango utakaowezesha kuzuia hujuma.
 
 Wananchi wakijua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, gharama yake na jinsi inavyotekelezwa, inaweza kuwa rahisi kufuatilia kama kilichokusudiwa ndicho kinachotekelezwa.
 
 Kama watabaini kuwa sicho, wanaweza kupaza sauti ili wahusika wachukuliwe hatua haraka, kuliko kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao bila wao kujua kinachoendelea.
 
 Yawezekana hawajui kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo ni ya serikali, hivyo hawahusiki kuifuatilia. Kama ndivyo wanavyodhani, basi waelimishwe ili wajue wajibu wao.
 
 Inasikitisha kuona miradi ya mabilioni ya fedha ikikataliwa. Chanzo cha kutekelezwa chini ya kiwango ni ili sehemu ya fedha za mradi hiyo iingizwe kwenye mifuko na kuishia kwenye matumbo ya wachache.
 
 Lakini kama wananchi wangejua kuwa miradi hiyo ni yao na wanatakiwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake, pengine kusingekuwa na taarifa za kukataliwa, kwani yote ingetekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa.
 
 Hivyo, ingependekezwa kuwa kama wananchi watashirikishwa kikamilifu, hasa kwa kupewa elimu ya kujua muhimu wa kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili nao waweze kuifuatilia, kukosoa na kuripotri upungufu.
 
 Vinginevyo, hujuma katika miradi ya maendeleo inaweza kuendelea, kwani sidhani kama mwananchi anayejua umuhimu wa miradi ya maendeleo katika eneo lake anaweza kunyamazia hujuma.
 
 Ikumbukwe kuwa, dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, lakini inapokataliwa, ni kwamba ina kasoro.
 
 Hujuma ni dhidi ya miradi ya maendeleo ni adui mkubwa ambaye anapaswa kupigwa vita na kila mpenda maendeleo, ili kodi za wananchi zitumike inavyotakiwa kwa ajili yao na taifa kwa ujumla.
 
 Lakini pia ni vyema TAKUKURU nao wakawa wanafuatilia miradi hiyo tangu mwanzo ili iwe rahisi kubaini udanganyifu unaofanyika badala ya kusubiri kupelekewa taarifa ili wachunguze.
 
 Kwa mtazamo wangu, kusubiri kupelekewa taarifa mezani ili waanze kuchunguza, kunawapa mwanya wajanja wachache kuendelea kufanya hujuma kwenye miradi na kujiimarisha kwa ajili ya kuficha ushahidi.
 
 Maelekezo ambayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahi kuyatoa kwa wakuu wa mikoa na wilaya, ni kwamba wasimamie miradi yote ya maendeleo kwenye maeneo yao na kuhakikisha inakamilishwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.
 
 Katika maelekezo yake zaidi ni kwamba eneo la usimamizi wa miradi, wahakikishe wana taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo, wajiridhishe kama imekamilika au la, na kama bado haijakamilika, wafuatilie ili kujua ni kwa nini haijakamilika.
 
 Ufuatiliaji unaweza kuja na majibu mazuri kwani unasaidia kujua kama kuna hujuma au uzembe. Lakini ushirikishwaji wa wananchi kudhibiti hujuma katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao ni la muhimu.