Kuna udhaifu wa wapiga faulo kwenye soka letu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:40 AM Oct 28 2024
Kuna udhaifu wa wapiga faulo kwenye soka letu
Picha: Mtandao
Kuna udhaifu wa wapiga faulo kwenye soka letu

INAONEKANA kuna matatizo ya 'maspesholisti' wa kupiga mipira iliyokufa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na soka la nchi hii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa takwimu za Kitengo cha Dawati la Michezo la Nipashe, kati ya mabao 135, yaliyofungwa mpaka leo hii kwa msimu huu, ni sita tu yamefungwa kwa mipira ya faulo za moja kwa moja.

Kwa maoni yangu, ni kiwango kidogo mno kwa idadi ya mabao ambayo yamefungwa mpaka sasa.

Takwimu zinaonesha kuwa winga wa Fountain Gate, Dickson Ambundo, ndiye anayeongoza akiwa amefunga mawili, Clatous Chama wa Yanga, Redemtus Mussa wa KMC, Ezekia Mwashilindi wa Prisons, Said Ndemla wa JKT Tanzania  wote wamefunga bao moja moja.

Kwa Ligi Kuu kama ya Tanzania kuwa na idadi hiyo ya mabao ya mipira iliyokufa, inaonesha kuna matatizo sehemu ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi.

Inawezekana kwa miaka ya hivi karibuni hakuna wachezaji wenye vipaji vya kupiga mipira ya faulo kama ilivyokuwa zamani.

Nikirejea miaka ya nyuma kuanzia 1980 hadi 1990, kulikuwa na wachezaji waliokuwa na uwezo mkubwa wa kupiga faulo zilizokuwa hatari na mara nyingi zikizaa mabao.

Fred Felix Minziro wa Yanga alikuwa mmoja wa wachezaji wenye uwezo huo, kiasi cha staili yake ya upigaji kupachikwa jina la 'banana chop' kwani ilikuwa ni hatari sana, mpira ulikuwa unazunguka na kupinda kama ilivyo ndizi, hata kama akikosa, lakini kizaazaa lazima kiwapo langoni.

Wengine ni Ahmed Amasha wa Yanga, upande wa Simba alikuwa ni George Lucas, Hussein Masha na hata timu za mikoani zilikuwa na wachezaji ambao walikuwa ni maalum kwa mipira hiyo.

Na siyo faulo tu, hata kona pia kulikuwa na watu maalum, ambao zilipokuwa zinapigwa na kuzaa hatari sana langoni mwa timu pinzani.

Inawezekana pia wachezaji wa kisasa ni wavivu kufanya mazoezi ya kupiga faulo tofauti ya wale za zamani na hata nje ya nchi.

Tunaona baadhi ya wachezaji kwenye ligi za nje, wakifanya mazoezi ya faulo kwa saa nyingi kiasi kwamba timu yake ikipata faulo, si kama anakwenda kujaribu, bali kukifanyia kazi kile achokifanyia mazoezi.

Inawezekana pia ikawa walimu wengi na makipa wameshajua mbinu za wapigaji, hivyo kuweza kujipanga vema na kutoleta hatari.

Pamoja na yote hayo, ikumbukwe kuwa faulo ni moja kati ya njia ya kupata mabao kirahisi kwenye mchezo wa mpira wa miguu, kama timu itakuwa na mpigaji mzuri au wachezaji kujifunza namna ya kuwahadaa wapinzani wakati wa kupiga.

Mimi naona kama wachezaji wengi hufanya mzaha sana linapokuwa suala la kupiga faulo, lakini ni moja kati ya nafasi nzuri mno za kupachika mabao.

Inawezekana timu ikashindwa kupata nafasi dakika 90 za mchezo, lakini ikapata faulo hata nne ambazo zikitumiwa vema zinaweza zikazaa bao moja au mawili yanayoweza kuamua mechi.

Miaka ya katikati ya 1990, Simba ilipokuwa ikifundishwa na Dragan Popadic aliyekuwa raia wa Yugoslavia kwa wakati huo, sasa Serbia, aliweza kuifanya timu hiyo kuwa hatari mno kwenye mipira iliyokufa na kona.

Simba ilitwaa ubingwa mwaka huo na mabao yao mengi yalikuwa yakifungwa kwa kona na faulo, kiasi cha kuwatisha mpaka wapinzani kucheza rafu karibu na eneo la hatari na pia kuhofia kutoa kona.

Kocha huyo alikuwa na mafunzo maalum ya mipira iliyokufa na kona, akitumia mpaka ringi la basikeli kufunga pembeni juu ya lango na kuwataka wachezaji wapige faulo kupitisha katikati ya mzunguko wa ringi. Hii iliifanya timu iwe ya kutisha na iliweza kupata mabao kwa njia yoyote waliyoihitaji.

Kwa sasa, pamoja na kuonekana kupungua kwa vipaji na uvivu wa wachezaji, lakini pia hata mafunzo ya mipira iliyokufa kutoka kwa walimu imekuwa finyu. Wanatumia wale ambao angalau wanaonekana wana uwezo tu wa kupiga faulo na kuweza kulenga lango waamue.

Nchini Afrika Kusini kwa sasa Klabu ya Mamelodi Sundowns, imeajiri makocha wa kufundisha kupiga faulo na pia kuzuia kufungwa aina hiyo ya mipira.

Nadhani hata hapa nchini kwa sasa wanahitajika, kama si kwenye klabu, basi hata Shirikisho la Soka nchini (TFF), liwaajiri kwa ajili kufundisha vijana wanaochipukia kwenye kituo chake cha malezi, ili baadaye nchi irejee kuwa na wapiga faulo wa kuaminika kama zamani.