Yanga kushusha beki la Enyimba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:07 AM Jun 26 2024
Chikamso Okechukwu.
Picha: Mtandao
Chikamso Okechukwu.

KATIKA kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, Yanga imepiga hodi Klabu ya Enyimba kutaka kumsajili beki wa kati wa timu hiyo, Chikamso Okechukwu, mwenye umri wa miaka 22.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa tayari viongozi wa Yanga wameanzisha mazungumzo na wenzao wa Enyimba kuona uwezekano wa kuipata saini ya mchezaji huyo kwani bado ana mkataba na kikosi hicho cha Mabingwa wa Afrika 2003.

Beki huyo raia wa Nigeria anatajwa kuja kuchukua nafasi ya Gift Fredy raia wa Uganda ambaye ameshindwa kumshawishi Kocha Miguel Gamondi tangu alipojiunga kutoka SC Villa ambapo amekuwa hana namba ya kudumu ndani ya kikosi hicho.

"Hapa kuna mawili, anasajiliwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Gift, pia hakuna uhakika sana kama Mwamnyeto (Bakari), atabaki japo mazungumzo yanaendelea, lakini hata kama akibaki, Okechukwu anatakiwa kwa udi na uvumba, labda dili liharibike mwishoni.

Kocha anataka mara nyingi Dickson Job acheze pembeni na siyo kati kwa sababu ya hatari ya mipira ya juu, kati pale acheze lakini isiwe ndiyo namba yake ya kudumu, anamtaka beki mrefu aje kutengeneza pacha na Bacca (Ibrahim Hamad).

Okechukwu ndiye beki tegemeo kwa sasa kwenye kikosi cha Enyimba ambacho kilimaliza ligi kikiwa nafasi ya tatu Ligi Kuu ya Nigeria msimu uliomalizika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa sasa hawawezi kuweka wazi wachezaji ambao imewasajili au kuwaacha mpaka itakapofika Julai Mosi kama alivyoahidi huko nyuma.

"Ikifika Julai Mosi, sisi Yanga ndiyo tutarudi mzigoni, sasa hivi tuko mapumzikoni, tunainjoi likizo zetu, lakini ikifika siku hiyo tunaanza kuvaa sura ya kazi. Tutaanza maboresho ya kikosi chetu cha msimu wa 2024/25, pia kuwatangazia wanachama na mashabiki wa Yanga ratiba nzima ya 'pre season' yetu, sasa hivi tuacheni tu tule bata kwa sababu ya kazi kubwa ambayo tumeifanya msimu uliomalizika.

"Wanachama na mashabiki wa Yanga wala wasiwe na wasiwasi, ikifika siku hiyo tutaanza kutangaza idadi ya wachezaji ambao watasalia kwenye kikosi, kutoa taarifa ya wachezaji ambao wanaondoka, lakini kuwajulisha majembe mapya ambayo yameingia ndani ya kikosi chetu," alisema Kamwe.