Simba, straika wa Asante Kotoko safi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:18 AM Jun 26 2024
Steven Mukwala.
Picha: Mtandao
Steven Mukwala.

KLABU ya Simba imetajwa kumalizana na straika Steven Mukwala anayekipiga na Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana kwa ajili ya kutibu tatizo sugu la kupachika mabao.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa mchezaji huyo amepatikana kutokana na maskauti walioteuliwa na Mwekezaji, rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed 'Mo' Dewji, ambaye safari hii ameingia kazini mwenyewe kuhakikisha wachezaji bora wanapatikana.

Chanzo hicho kimebainisha kuwa straika huyo anaweza kutibu tatizo la ushambuliaji ndani ya klabu hiyo, kwani pamoja na kuwa tegemeo kwenye klabu hiyo, lakini anaichezea Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes.

"Nadhani ni chaguo sahihi, ana miaka 24 sasa, huyu kijana ndiye alikwenda kumaliza utawala wa kina Emmanuel Okwi na Farouk Miya kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda, uzuri na yeye ameonekana kufurahia kuchezea Simba kutokana na rekodi nzuri ya wachezaji wa timu hiyo walioichezea miaka ya nyuma.

"Ameongea na kina Okwi na Patrick Ochan ambao walicheza Simba na kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja kwa hiyo na yeye amevutiwa, ndiyo maana klabu yake ilitaka kumwongezea mkataba kabla ya msimu kumalizika lakini mwenyewe alikataa," alisema mtoa taarifa wetu.

Habari zinasema ushawishi wa wachezaji hao ndiyo kwa kiasi kikubwa umemfanya kuichagua Simba badala ya FC Petrocub ya nchini Moldovia ambayo mara kwa mara huwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua za awali.

Licha ya timu yake kumaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi ya Ghana, Mukwala amemaliza akiwa nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora nchini humo, akipachika mabao 14, akiongozwa na mshindi wa kiatu cha dhahabu msimu uliomalizika, Stephen Amankona wa Berekum Chelsea FC alimaliza na mabao 19.

Straika huyo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Pa Omari Jobe ambaye taarifa zinaeleza kuwa atatolewa kwa mkopo baada ya kushindwa kuonyesha makali yake tangu aliposajiliwa katikati ya msimu uliomalizika.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watulivu kwani kila mchezaji aliyesajiliwa atatangazwa kwa nyakati tofauti, akitamba kuwa safari hii wanafanya usajili mkubwa.

"Muda utaongea, tumeshaanza kutoa 'thank you', kutangaza wachezaji wapya tuliowasajili, na tunaowaongeza mikataba, kwa hiyo yeyote ambaye tumemsajili tutamtangaza wenyewe, mashabiki wavute subira, safari hii Mo mwenyewe ndiye anaongoza kikosi cha usajili, hii inadhihirisha kuwa meshine zitakazoshuka zitakuwa ni mashine kweli kweli," alisema.

Wakati huo huo, klabu hiyo imetangaza rasmi kumwongeza mkataba wa miaka miwili mingine kiungo wake, Mzamiru Yassin.

Kiungo huyo amekuwa na timu hiyo kwa miaka minane sasa, tangu alipojiunga nayo mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar.