Simba SC, Coastal zamgombea Lawi

By Faustine Feliciane ,, Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 07:19 AM Jun 22 2024
news
Picha:Mtandao
Lameck Lawi.

WAKATI Simba ikitangaza itaenda kuweka kambi yake katika jiji la Ismailia, Misri, mabosi wa klabu hiyo wamesema walifuata taratibu zote katika mchakato wa kumsajili beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi, imefahamika.

Uongozi wa Coastal Union umesema Lawi bado ni mchezaji wao halali na wanashangaa kuona Simba imemtangaza beki huyo kuwa ni mali yake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, alisema klabu hiyo ililipa awamu ya kwanza ya fedha kwa Coastal Union na kiasi kilichosalia walitakiwa kukikamilisha Mei 31, mwaka huu.

Magori alisema Coastal Union ilipaswa kuandika barua ndani ya siku 10 endapo Simba ilichelewa kukamilisha malipo lakini haikufanya hivyo.

Kiongozi huyo alisema Simba ilifuata taratibu zote na ilikamilisha malipo ya awamu ya pili ndani ya muda.

"Huu mpira ni wa FIFA, haushii Karume (ilipo Shirikisho la Soka Tanzania- TFF), hawa wameingia tamaa baada ya mchezaji kupata timu nje, sasa wamuuze, tutawashitaki Coastal pamoja na timu itakayomnunua," Magori alisema.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisisitiza  wamemalizana na mchezaji huyo kwa kumpa mkataba wa miaka mitatu na tayari wamelipa kiasi chote cha fedha walichotakiwa na mabingwa hao wa mwaka 1988.

Hata hivyo Ahmed aliongeza Simba imeanza mchakato wa kusaka beki mwingine wa kati ili kuungana na Lawi kikosini hapo.

"Tumeshampata Lawi, kikosini tuna Huseein Kazi , tuna Che Malone na sasa tunataka beki mwingine wa kati ambaye tutamtangaza hivi karibuni kwa ajili ya  kukiimarisha kikosi chetu, tumepania sana msimu ujao," alisema Ahmed.

Aliongeza bado hawajamaliza kutangaza wachezaji wanowaacha kwa sababu wanataka kuongeza 'majembe' yatakayokuja kuendeleza mazuri ndani ya kikosi chao.

"Tulisimama kuendelea kutangaza nyota tunaowaacha kwa sababu tulitaka kuwabadilishia ladha mashabiki kwa kumtangaza mchezaji wa kwanza tuliyemsajili, sasa tunarejea tena kuwatangaza tunaowaaga," alisema Ahmed.

Naye Msemaji wa Coastal Union, Abbas El Sabri, aliiambia gazeti hili, Lawi bado ni mchezaji wa Coastal Union baada ya Simba kutofuata taratibu walizopeana katika kumsajili beki huyo.

"Huo usajili tunausikia tu katika mitandao, Lawi ni mchezaji wetu, ni kweli Simba walileta ofa na sisi tukawapa utaratibu wetu kukamilisha usajili huo, lakini sijui walikutwa na nini hawakufuata huo utaratibu, tulipoona wenzetu wanachelewa tukakaa na mchezaji na kumweleza mipango yetu na kuamua kubaki naye kikosini, Lawi bado mchezaji wetu," alisisitiza El Sabri.