Nyota Stars awaita wadhamini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:31 AM Jun 22 2024
Mchezaji wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Novatus Dismas (20).
Picha: Godfrey Mushi
Mchezaji wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Novatus Dismas (20).

MCHEZAJI wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Novatus Dismas (20), anayecheza katika Klabu ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine, amefungua rasmi michuano ya East African Cup akimwomba, Rais Samia Suluhu Hassan, kuifadhili ili kuibua vipaji vya wachezaji chipukizi.

Novatus, ambaye kipaji chake kiliibuliwa kupitia mashindano hayo, alifungua michuano hiyo jana, inayoendelea kwenye Shule ya Ufundi Moshi.

Nyota huyo ameliomba pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuitizama michuano hiyo na kuisapoti, kwa sababu vijana wengi wenye vipaji watapatikana na kuja kulisaidia taifa katika mashindano mbalimbali ikiwamo Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Ni ushauri na ombi pia kwa watu wanasiasa, na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwashika vijana mkono vijana ili waweze kufikia malengo yao. 

Kuwa na mashindano mengi kama East African Cup, ni kitu kizuri ambacho kitawafanya vijana wapate fursa ya kuonekana na kupata nafasi katika sehemu mbalimbali," alisema Novatus.

Mratibu na mwandaaji wa michuano hiyo, Prisca Lema, alisema mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka mkoani Kilimanjaro, mwaka huu yameshirikisha timu 28.

“Tuna wachezaji wa umri chini ya miaka 13 na 16 kwa wasichana na wavulana. Kwa mwaka huu kuna mchezo mpya tutauanzisha ambao ni mpira wa kikapu.

East African Cup, imekuwa ni moja ya jukwaa kubwa ambalo linaibua vipaji kwa vijana wa kike na wa kiume lakini pia marefa na makocha ambao wanafanya vizuri sana nchini Tanzania," alisema mratibu huyo.