Mazoezi Twiga Stars yakolea

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 07:31 PM Jul 04 2024
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime.
Picha: TFF
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime.

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime, amesema anafurahishwa na ushindani uliopo katika kikosi chake kinachojiandaa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Tunisia na Botswana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Shime, alisema kila mchezaji anajituma kwenye mazoezi kwa sababu hakuna nyota ambaye ana uhakika wa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Shime alisema hali hiyo inasaidia kuimarisha ubora wa wachezaji wake na anakuwa na kikosi kipana.

"Kila mchezaji anajituma na anaonyesha juhudi, mazoezii yanaendelea vizuri, tunaamini timu yetu inazidi kuimarika, ujio wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa unasaidia kuongeza uzoefu," Shime alisema.

Wachezaji walioitwa kujiandaa na mechi hizo za kirafiki ni Najat Abasi kutoka JKT,  Asha Mrisho (Amani), Lidya Maximilian (JKT), Protasia Mbunda (Fountain Gate), Enekia Kasonga (Eastern flames), Julietha Singano (Mexico), Vailet Mwamakamba (Simba Queens), Anastazia Katunzi, Joyce Lema na Janeth Christopher  wa JKT.

Wengine ni Ester Maseke kutoka Bunda, Diana Lucas (Ame SKF), Aisha Juma (Simba Queens), Stumai Athumani, Winifrida Gerald (JKT), Maimuna Kaimu (ZED ya Misri), Elizabeth Charles ( Alliance), Aisha Masaka (BK- Hacken), Oppa Clement (Besiktas), Clara Luvanga (Al Nasr- Saudi Arabia), Victoria Maselle (TopHat Soccer Academy -Georgia) na  Malaika Meena kutoka Forest University ya Marekani.

Twiga Stars imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), ambayo yamesogezwa mbele na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hadi Julai mwakani.