Kisinda atajwa kutakiwa Coastal Union 2024/2025

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:25 AM Jun 22 2024
Tuisila Kisinda.
Picha: Mtandao
Tuisila Kisinda.

WAKATI ikianza kutangaza majina ya wachezaji inayowaacha, Coastal Union iko mbioni kumsajili winga wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda, lengo ikiwa ni kujiimarisha kuelekea mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, imefahamika.

Habari kutoka ndani ya Coastal Union zinasema mazungumzo na Kisinda yameshaanza, na endapo yakienda vyema, basi mchezaji huyo atamwaga wino katika klabu hiyo.

"Tunaendelea na usajili, na tunalenga wachezaji ambao ni wazoefu kwenye michuano ya kimataifa, huwezi kwenda kucheza huku ukiwa na vijana wengi, wakongwe, siyo wa umri, ila kwenye mechi kubwa wanahitajika, hivyo tunamkata Kisinda, najua atakuja kutusaidia kwa sababu amecheza klabu kubwa kama AS Vita, Yanga na RS Berkane," kilisema chanzo chetu.

Siku chache kabla ya taarifa hizi, Ofisa Habari ya Klabu hiyo, Abbas El Sabri, alikiri kufanya mazungumzo ya mchezaji mwingine raia ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Djuma Shaaban.

"Ni kweli tupo katika mazungumzo na Djuma, ni mchezaji mzuri, mzoefu katika mechi za kimataifa. Unajua tangu tulipopata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho, tayari kama klabu tukatambua mahitaji yetu yataongezeka, kuanzia gharama, wachezaji na hata muda utakuwa finyu," alisema El Sabri.

Mbali na huyo ambaye Coastal Union imekiri, lakini taarifa zinasema wanaendelea na mazungumzo na Saido Ntibazonkiza kama ambayo gazeti hili liliripoti hivi karibuni kabla ya hata ya kuachwa na Simba.

Wakati huo huo, klabu hiyo imeanza kutoa majina ya wachezaji inayoachana nayo, ambapo imewatangaza, Roland Beako na Aboubakar Abbas, hawatakuwa sehemu ya kikosi chao katika msimu mpya.

Kisinda amezichezea Yanga na RS Berkane ya Morocco kwa vipindi viwili tofauti kwa kila timu, akisajiliwa kutoka AS Vita mwaka 2021, akaenda RS Berkane mwaka 2022, lakini alirejeshwa kwa mkopo na mwaka jana alirejea kwenye klabu yake ya awali na sasa  amemaliza mkataba.