JKT Queens: Tutalinda heshima

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 08:26 AM Jan 10 2025
MSHAMBULIAJI wa JKT Queens, Winfrida Gerald.
Picha:Mtandao
MSHAMBULIAJI wa JKT Queens, Winfrida Gerald.

MSHAMBULIAJI wa JKT Queens, Winfrida Gerald, amesema atapambana kuhakikisha timu yake inapata ushindi katika kila mechi watakayocheza katika mashindano ya Wasichana ya CAF U-17 ( GIFT), yanayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Winfrida alifunga mabao mawili katika ushindi wa magoli 3-0 kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya KAS kutoka Kenya iliyochezwa juzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Winfrida, alisema licha ya mashindano hayo kuwa na upinzani, lakini wamejiandaa kufuata vyema maelekezo wanayopewa na kocha wao ili kutimiza malengo.

 "Malengo yangu ni kushinda michezo yote ili tuibuke mabingwa wa mashindano haya, tunaomba mashabiki waendelee kutuunga mkono, bila wao hatuwezi kufanya lolote," alisema mshambuliaji huyo.

Alisema wanashukuru kwa kuanza vyema michuano hiyo na wamejipanga kuendelea kusaka ushindi ili kusonga mbele katika michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza.

"Tulipata ushindi kutokana na kufuata vizuri maelekezo tuliyopewa nje na ndani ya uwanja kabla ya kuanza kwa mashindano, tutaendelea kupambana katika kila mechi, hatutadharau timu yoyote," alisema Winfrida.

Aliongeza anafurahishwa na ushindani unaonyeshwa na wasichana katika mashindano hayo jambo ambalo linampa matumaini ya kuona soka la wanawake linazidi Afrika Mashariki na Kati linakua.