Kituo mama cha gesi ya magari, bajaji kuanza kazi mwezi ujao

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:38 PM Jan 10 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko (wapili kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Meneja Msimamizi wa Mradi wa Kituo Kikuu cha Kujazia Gesi Asilia (CNG Mother Station) jana, kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDS).
Picha: Mauld Mmbaga
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko (wapili kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Meneja Msimamizi wa Mradi wa Kituo Kikuu cha Kujazia Gesi Asilia (CNG Mother Station) jana, kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDS).

KITUO Kikuu cha Kujazia Gesi Asilia (CNG Mother Station) kilichoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinatarajiwa kuanza kazi rasmi Februari 3 mwaka huu.


Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza magari 1,000 kwa siku, hivyo kusaidia kupunguza msongamano uliopo katika vituo vinne vilivyopo jijini Dar es Salama.

Kumekuwa na changamoto ya msongamano wa vyombo vya usafiri vinavyotumia mfumo wa gesi asilia, hasa bajabi na magari wakati wa kujaza gesi kutokana na uhaba wa vituo husika, jambo lililolazimu serikali kuongeza idadi ya vituo hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kinachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Naibu Waziri Mkuu Biteko alisema ujenzi wake umefikia asilimia 80 unaendelea vizuri na mitambo yote inayohitajika tayari imeshawasili nchini.

"Mkandarasi ametuhakikishia kwamba itakapofika Februari 3 mwaka huu kwa mara ya kwanza magari yataanza kwenda kujaza gesi hapa. Lengo letu ni kuondoa foleni ambazo mnaziona zinajitokeza hapa na pale kwa sababu mwitikio wa watanzania kuhamia kwenye mfumo wa gesi ni mkubwa.

"Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kwamba tujenge vituo vingi zaidi hapa Dar es Salaam ambayo ndiyo mtumiaji mkubwa wa gesi, hiki ni kituo kimojawapo lakini wakati huo huo vinajengwa vingine, saba mkoani hapa kupitia sekta binafsi," alisema Dk. Biteko.

Aliongeza kuwa nia yao ni kwamba ndani ya mwaka huu, waongeze vituo vingine kutoka vitatu vilivyokuwapo mwaka jana hadi kufikia 15.

Alisema kuwa pia kutakuwa na magari yanayotembeza gesi na kujaza katika magari mengine na bajaji katika mikoa ya Morogoro kimoja na viwili Dodoma, akisisitia kuwa wanataka kuwahamisha wananchi kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu kwenda safi.

Alisema wanataka kuongeza kasi na kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinajengwa kwa haraka, huku akiwapongeza TPDC kwa kazi nzuri waliyofanya katika kituo hicho mama ambacho wametoa ufadhili kwa asilimia 100.

Alisema Sh. bilioni 18.9 zinatumia kujenga kituo hicho pamoja na vingine viwili vya Kairuki wilayani Kinondoni na Muhimbili jijini Ilala.

Pia alionesha kufurahishwa na hatua ya TPDC kujengea uwezo kampuni binafsi pamoja na vijana wa ndani, akieleza kuwa asilimia 100 ya wafanyakazi katika ujenzi wa vituo hivyo ni wazawa, jambo lililosaidia pia kutengeneza ajira.

"Serikali haijalala, wakati wote tunahakikisha tunawapatia watanzania nishati safi hasa CNG ili kupunguza gharama ambayo ni kubwa sana unapotumia mafuta ya kawaida," alisema Dk. Biteko.

Meneja Msimamizi wa Mradi huo kutoka TPDS, Aristides Katto, alisema kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kusambaza gesi katika vituo vingine kupitia magari. Pia kitakuwa na pampu nne zitakazohudumia zaidi ya magari manane kwa pamoja.