Rais Samia kuzindua tamasha la kitaifa la utamaduni Julai

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:40 AM Jun 21 2024
RAIS Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mtandao
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua tamasha la Kitaifa la Utamaduni lililopangwa kufanyika kwa siku saba kuanzia Julai 20 katika viwanja vya Majimaji mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, alisema tamasha hilo litakuwa la kihistoria, litakusanya tamaduni kutoka mikoa yote Tanzania.

Alisema tamasha hilo linatokana na maagizo ya Rais Samia aliyotoa mwaka 2021 akiwa kwenye ziara mkoani Mwanza.

"Rais aliagiza kufanyika kwa tamasha la Utamaduni kila mwaka ili kurithisha Mali na Utamaduni wa kitanzania.

"Tanzania ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, tofauti yake inajenga Umoja na yanaunganishwa na Lugha ya Kiswahili.

"Kudumu kwa Utamaduni inategemea namna unavyorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na kwamba urithi wa Utamaduni ni kivutio kikubwa cha utalii, watalii wamevutiwa sana,"alisema Mwinjuma.

Aidha, alisema tamasha hilo litakuwa tofauti na matamasha mengine mawili yaliyowahi kufanyika mwaka 2022 na 2023 kwani litakuwa na sura ya Kitaifa na litakuwa chini ya Wizara husika.

Waziri Mwinjuma alisema jukumu la rasilimali fedha litakuwa chini ya Sekta Binafsi ambayo ni Kampuni ya DrumBeat Carnival  (Tz) Limited itakayosaidia pia kuhamasisha tamasha liwe na hadhi kubwa.