MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara umeanza, huku kila timu ikijidhatiti kupata matokeo mazuri ili kufikia malengo iliyojiwekea.
Kuna timu zitauhitaji ushindi kwa udi na uvumba, zipo zinazotaka kumaliza ndani tu timu nne za juu ili kupata angalau nafasi ya kucheza mechi za kimataifa mwakani na zile ambazo zitakuwa zinakusanya pointi kwa ajili ya kutaka kubaki Ligi Kuu.
Hata hivyo, ni lazima mwishoni zipatikane timu mbili zitakazoshuka daraja na mbili zitakazocheza mechi za mchujo. Lakini ni baada ya kufanya vibaya kwenye michezo ya Ligi Kuu hatua iliyobaki.
Tunataka timu zitakazoshuka na kwenda 'play off', ziwe kweli zimeshuka kutokana na uwezo wao mdogo na si kukandamizwa kwa sababu zozote zile.
Zitakazokwenda kucheza michuano ya kimataifa ziwe zilizofuzu kweli kweli na si kupelekwa kwa kusaidia, matokeo yake kwani timu nyingi zinatolewa mapema na kubaki chache, kitu ambacho si afya kwenye soka la Tanzania.
Hata bingwa, anatakiwa awe ni yule ambaye kweli ameupata kwa kuutolea jasho na si kubebwa na waamuzi ambao wakati mwingine wamekuwa wakilaumiwa kwa kuchezesha kinyume cha kanuni za soka duniani ama kwa upendeleo, woga, maagizo ama hata rushwa ambayo mara nyingi imekuwa vigumu kuthibitishwa, kitu ambacho kinazalisha kile kinachoitwa makosa ya kibinadamu.
Kwa maoni yetu, tunawataka waamuzi wote watakaochezesha mechi za mzunguko wa pili wachezeshe kwa makini na haki, bila kuipendelea au kuionea timu yoyote.
Klabu hizi tunaziona zimekuwa zikihangaika kupata makocha wazuri kwa kuwalipa pesa nyingi, kufanya usajili mzuri, lakini wakati mwingine wanaangushwa na kosa moja la mwamuzi ambalo wakati mwingine linasababisha si timu kupoteza mechi, bali hata makocha kutimuliwa.
Hiki ni kipindi hatari cha makocha ambao wataonekana hawafikii malengo ya timu kutimuliwa, sasa waamuzi wasiwe ndio chanzo cha kuwakosesha wenzao mkate kwa manufaa yao, uzembe, au kutokuwa makini.
Tunaona itabidi waachwe makocha watimuliwe kutokana na kushindwa wao wenyewe, si kwa mtu mwingine kumfanya aonekane hawezi, hii kwetu ni dhambi kubwa na haivumiliki.
Kwa waamuzi wenyewe angalau husimamishwa na baadaye kurudishwa uwanjani, lakini makocha wakishatimuliwa hawawezi kurudishwa tena kwenye klabu ile, badala yake atakaa ili kuona ni sehemu gani anahitajika, wakati mwingine hili huchukua muda mrefu, huku akiwa hana kazi yoyote.
Viongozi wa klabu hata zile zinazoitwa au kujiinda ndogo, mzunguko huu wa pili zimeonekana kujitutumua kusajili wachezaji wazuri na baadhi ya makocha bora kutoka ndani na nje ya nchi, tunadhani sasa ni wakati wa kuuacha mpira wenyewe uchezeke kiwanja na uamue nani mshindi kwa uwezo na si vinginevyo.
Kinyume cha hayo ni kutozitendea haki klabu na viongozi wao, ambao huingia gharama kubwa ya kuwalipia vibali vya kazi na ukaazi wachezaji wa nje kwa ajili ya kuzipigania timu zao, halafu mwamuzi anakuja kuingia na matokeo yake mfukoni.
Tunawashauri waamuzi waingie uwanjani kama mahakimu wa haki na haki ionekane ikitendeka kweli, kwani kwa tunavyojua mzunguko wa pili utakuwa mgumu mno na ushindani mkubwa, pointi moja tu iliyopatikana au kukosekana kwa makosa ya refa, inaweza kuipatia timu ubingwa isiyostahili, au kuinyima iliyotakiwa iupate.
Lakini inaweza kuishusha timu daraja ambayo ilitakiwa kubaki, kuibakisha iliyostahiki kwenda Ligi ya Championship, vile vile kuzipa timu dhaifu nafasi za kucheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho na kuziacha ambazo zingekwenda kuliwakilisha vema taifa.
Bingwa bora, wawakilishi wa nchi, zikazoshuka daraja na kubaki, wote wako kwenye mikono ya waamuzi watakaoamua kuchezesha kwa kufuata sheria zote 17 soka ulimwenguni. Hivyo tunazitakia timu zote kila laheri kwenye mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara huku tukitaka 'Mchezo wa Haki (Fair Play), kama kaulimbiu ya Fifa inavyosema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED