WAKATI tukiwa tunaelekea mwisho wa mwaka, ajali nyingi zimetokea na kumaliza uhai wa watu wengi ambao walikuwa ni tegemeo kubwa kwa taifa katika uzalishaji.
Katika miezi ya kuanzia Agosti, Septemba na sasa Oktoba ukiingia ukingoni, ajali nyingi za barabarani zimetokea na watu wengi wamepoteza maisha.
Ajali zinazoripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari idadi yake inatisha na kwa kweli inaacha simanzi kubwa kwa familia.
Matukio haya ya ajali mara nyingi yakifuatiliwa unakuta ni uzembe wa madereva na kutozingatia alama za usalama barabarani.
Baadhi ya madereva wanapokuwa barabarani hawajali kama kwenye magari wanayoyaendesha wamebeba roho za watu ambao wanategemewa na familia zao.
Hata hao madereva wenyewe wanapofanya uzembe huo hawajali kuwa na wao pia wapo kwenye hatari ya kupoteza maisha.
Kila mara askari wa usalama barabarani wamekuwa wakitoa elimu ya madereva kuzingatia usalama wawapo barabarani, lakini elimu hiyo haitiliwi maanani.
Pamoja na serikali kuamuru mabasi kuwekwa vidhibiti mwendo, lakini madereva wanavichezea na wanapokuwa kwenye masafa marefu wanakwenda kwa mwendo ule ule wa hatari.
Wakati taifa likiwa bado kwenye maombolezo ya vifo kadhaa vilivyotokea kwenye ajali siku chache zilizopita, kabla machungu hayo hayajapoa, ajali nyingine imetokea na kupoteza watu kadhaa na kuacha wengine wakiwa na majeraha na baadhi kubaki na ulemavu wa maisha.
Ajali hizi zitaendelea kutokea mpaka lini, ni lini madereva watakuwa na uelewa wa kuendesha magari yao kwa kuzingatia sheria za barabarani.
Wakati mwingine dereva wa gari lingine anaweza kuwa makini kwa kufuata sheria, lakini anakuja kugongwa na dereva mzembe anayeonesha mbwembwe barabarani.
Mwendokasi mara nyingi ndio unaosababisha ajali nyingi kutokea na hii inatokana na madereva hao kutaka kuwahi ili aende tripu nyingi zaidi.
Hata maeneo ya mjini mtu anaendesha kwa mwendo wa kasi bila kujali kuwa linapotokea tatizo la dharura atashindwa kudhibiti gari lake.
Kuna wakati ilishuhudiwa gari likiwa limeparamia mti na kuning’inia juu, kila mtu aliyepita eneo lile alibaki akijiuliza imekuaje yule dereva mpaka akapanda pale juu ya mti.
Kwa kweli hali inazidi kuwa mbaya na pia safari za usiku zimeanza kuleta madhara baada ya ajali nyingi kutokea muda huo, pengine kwa madereva kuchoka na kusinzia na wengine kabla ya kuanza safari kunywa vilevi, hali inayosababisha washindwe kuendesha kwa umakini vyombo vyao.
Juzi tu tumepoteza wanakwaya watano eneo la Kirinjiko, Same mkoani Kilimanjaro baada ya kupata ajali wakati wakienda kumzika mwanakwaya mwenzao.
Inasikitisha kuona wale waliokwenda kumzika mwenzao na wao wanapoteza maisha kabla hata ya kumlaza mwenzao kwenye nyumba yake ya milele.
Sijui kwa nini ajali zinapotokea zinakuwa na kisingizio cha mwisho wa mwaka. Madereva lazima wawe makini kwa kuendesha kwa umakini. Zingatieni alama za usalama barabarani, msiendeshe kwa mwendo zaidi ya ule unaoelekezwa barabarani. Huo mwendokasi ambao dereva lengo lake ni kufika haraka matokeo yake huishia kumaliza safari kabla ya mwisho wa kituo na kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Tumechoka kusikia kila siku taarifa za ajali zinazotokea na kumaliza nguvukazi ya taifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED