Mji wa aina yake uliojengwa juu ya meli zilizozama enzi hizo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:18 AM Nov 21 2024

Sehemu ya mji wa Baku ulioko juu ya bahari, nchini Azerbaijan.
PICHA: MTANDAO
Sehemu ya mji wa Baku ulioko juu ya bahari, nchini Azerbaijan.

NI miongo saba na nusu imepita sasa, eneo katikati ya Bahari ya Caspian kuna kisiwa kilichojengwa kwa nguvu na mkono wa mwanadamu, juu ya bahari.

Nyenzo zake ni nguzo za minara ya chuma ya kustaajabisha, mabomba, madaraja ya mbao, majengo ya kutoka enzi ya Jamhuri ya Kisoviet (USSR), ambazo hazionekani kwenye ramani.

Historia yake ilianza miaka ya 1940, wakati mtawala Joseph Stalin, aliamuru kufanyike ujenzi, baada ya kugundua kulikuwapo mafuta chini ya bahari ya Caspian.

Ni mahali umbali wa kilomita 55 kutoka eneo la Baku, mwambao uitwao Azerbaijan, ikiwa na maana Kirusi ‘Miamba ya Mafuta’ pakiweka rekodi kuwa mji wa zamani zaidi katika ukanda wa pwani hiyo kunakozalisha mafuta na umejengwa kwa teknolojia ya aina yake.

Hapo ndipo kuna mji wa Baku, penye kongamano la 29 la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2024, COP 29, likifanyika na kutarajiwa kumalizika wiki ijayo. 

UJENZI ULIVYOKUWA

Ilikuwa 1920 Jeshi la Kisovieti liliingia Azerbaijan na kuufanya sehemu ya USSR (Muungano wa Soviet) na ikadumu kuwa nayo hadi Oktoba 1991, muda mfupi kabla ya kuvunjika kwa muungano huo.

Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ilikuwa muhimu kwa mkakati wa kupata nishati kwa USSR, kwani mafuta mengi yaliyotumiwa na kambi ya Mashariki yalitoka Baku.

Awali eneo Neft Dashlari, iliandaliwa kuwa sehemu ya mradi wa miaka mitano uliosimamiwa na mtawala Joseph Stalin, ukiwa sehemu ya miradi ya maendeleo ya uchumi wa USSR wakati huo.

Ilikuwa alama ya usimamizi wa Kisoviet, ingawa mingi haikukamilishwa kutokana na ama kuachwa au kushindikana.

Ujenzi wake ulianza baada ya uchunguzi wa kwanza wa mafuta uliofanikiwa Novemba 7, 1949. Eneo lililogeuzwa kuwa moja ya hifadhi kubwa zaidi ya mafuta katika Asia ya Kati na kisima hicho kilitoa mafuta mengi (tani 100 kwa siku), kuashiria uzalishaji wa kwanza 

Azerbaijan inabaki kihistoria, ndiyo ya kwanza kuchimba mafuta katika sehemu ya wazi ya Bahari ya Caspian, kwa mujibu wa tovuti ya Socar, mmiliki wa kampuni ya mafuta ya serikali ya nchi hiyo.

Kile ambacho awali kilikuwa eneo ndogo la uchimbaji na nyumba ndogo ya wafanyakazi kukaa huko, kilibadilika kuwa ujenzi mkubwa kuanzia mwaka 1951, ukiitwa “muujiza wa usanifu na kiufundi."

MSINGI MELI MBOVU 

Ili kuharakisha ujenzi eneo hilo la pwani, kuna ufundi wa ziada ulifanyika kupitia  meli zilizokataliwa, zilizamishwa na kutumika kuwa msingi, juu yake nguzo za majengo zilisimikwa.

Mojawapo ya meli hizo ilikuwa aina yake ya mafuta ya kwanza kuwahi kutengenezwa duniani. 

Muundaji wake, Ludvig Nobel - kaka wa Albert Nobel, ametengeneza kama suluhisho la kusafirisha mafuta mwishoni mwa karne ya 19.

"Mnamo 1951 ili kulinda kisiwa hicho kutokana na upepo na mawimbi, meli sita za ziada za kampuni za Khazartanker na Khazardonanma zilibomolewa na kuletwa hapa, zikiwa zimezama nusu na ghuba ya bandia iliundwa kuzunguka kisiwa hicho.

Vyumba vya kuhifadhi meli vilifanywa ukumbi wa mlo, kituo cha matibabu, sehemu ya malazi na matumizi mengine kwa wafanyikazi wachimba visima.

Kwa mujibu wa tovuti ya Socar, hapo ndipo asili ya mji huo kupewa jina ‘Kisiwa cha Meli Saba.’Baadaye kisiwa hicho cha bandia kilijulikana kwa jina lake la sasa.

Kwa miaka mingi, eneo la Neft Dashlari, ilipanuliwa kuwa jiji kubwa mfano wa umbo la pweza juu ya bahari, kukiwapo vitalu vya ujenzi kwa wafanyakazi, duka la mikate, maduka, vituo vya matibabu, uwanja wa mpira wa miguu, helikopta na hata ukumbi wa michezo.

Ni kwa mujibu wa Mirvari Gahramanli, Mkurugenzi wa Shirika la Kulinda Haki za Wafanyakazi wa Mafuta linalosimamia haki za binadamu katika sekta ya mafuta na gesi ya Azerbaijan.

MJI ULIVYO

Mji huo unatajwa kujengwa mita kadhaa juu ya uso wa bahari na nguzo za chuma zilizowekwa chini ya bahari.

Kunaelezwa kuna majengo ya makazi, idara ya matibabu na usafi na maduka, pia miti imepandwa kwenye vizimba vya chuma na bustani zilizotengenezwa.

Eneo la Oil rocks, lina urefu wa kilomita 12 na upana wa kilomita sita, kulingana na data za asasi ya Gahramanli. Hapo kuna takribani visima 2,000 na wastani wa kilomita 200 za njia zimechimbwa eneo hilo.

Mwanzo kulikuwapo wakati kunaundwa kulikuwapo wafanyakazi wastani 5,000 na sasa kwa mujibu wa Gahramanli, wafanyakazi wako 3,000, ambao mtindo wao wa maisha wanatumia siku 15 baharini na siku 15 nyinginezo kwa mwezi wanakuwa nchi kavu.

TAASISI HUSIKA

Inatajwa Neft Dashlarim ni kampuni inayomilikiwa na asasi ya Socar chini ya miliki ya serikali ya Azerbaijan kunakofanyika mkutano wa Cop 29, ikijishughulisha na uzalishaji, usindikaji na usafirishaji mafuta na gesi, pia inauza bidhaa za mafuta, gesi.

Inaelezwa, kisiwa hicho kilikuwa na manufaa makubwa katika uzalishaji mafuta, ikitoa wastani wa tani milioni 180 za mafuta katika miaka 75 ya kuwapo kwake.

Katika kilele chake mwaka 1967, ilivuka rekodi ya tani milioni 7.6, sasa ikiwa katika tani 3,000 kulingana na takwimu zilizotolewa mnamo Januari mwaka huu.

Kihistoria, kisiwa hicho kilifanikiwa sana katika uzalishajii mafuta miaka ya 1960, lakini kuanzia muongo uliofuata, miaka 1970 hali ikabadilika.

Inatajwa sababu ni kubadilika bei ya mafuta na kuanza kuporomoka thamani ya fedha Dola ya Kisovieti, thamani yake ilianza kupungua.

Pamoja na mageuzi makubwa katika miaka mingi ya kuwapo, alipoulizwa kuhusu hatari ya kisiwa hicho kuzama kutokana na muundo wake au mabadiliko ya hali ya hewa, Mirvari Gahramanli akajibu: “Kisiwa hakiko karibu kuzama na hakuna hatari kama hiyo kwa sasa.”

Kimsingi hadi sasa, Neft Dashlari ni kituo cha kimkakati kilichoko baharini, chenye visima na kunafanyika uchimbaji na ujenzi, mitambo.

Inatajwa ikawezekana kufikika kwa helikopta au mashua, ila kwa asili yake, sio mahali panakofika kirahisi au kwa watalii. 

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa, unaelezwa katika ripoti iitwayo ‘Communications Earth & Environment’, huenda ifikapo mwaka 2100 (miaka 76 ijayo), kisiwa kitaporomoka kwa mita 18, sawa na asilimia 34 eneo la Bahari lililoko.

Katika utafiti huo, wanasayansi walionya maji hayo yatashuka kati ya mita tisa na 18 ifikapo mwisho wa karne iliyopo, hapo kukiendelea utoaji gesi na hewa chafu katika viwango vya sasa.

Hiyo inatokea huku, kikao cha hali ya hewa duiniani kinachoandaliwa na Umoja wa Mataifa- COP 29, kiko hapo kinajadili mada hiyo, ikiwamo ajenda  ya hali ya hewa ya sasa na baadaye duniani.

Rais mteule wa Azerbaijan, Mukhtar Babayev, anasema kuwa "juhudi za kila mtu" zitahitajika.

·                Kwa mujibu wa taarifa za kimataifa.