HADI sasa mpango wa serikali nchini ifikapo mwaka 2030 ni kuwa na umeme wa zaidi ya megawati 5,000 kutoka vyanzo tofauti, ikiwamo kutoka kwenye nishati jadidifu za jotoardhi, jua na upepo.
Hayo ni miongoni mwa mambo kadhaa yaliyoelezwa mjini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita, kwenye Kongamano la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) lililokusanya washiriki 800 kutoka nchi 21 duniani.
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango katika ufunguzi wa kongamano hilo, akaeleza kwamba ili kufanikisha hayo, serikali inatoa mwaliko kwa wawekezaji kutoka nchi mbalimbali, kuja nchini kuwekeza kwenye sekta ya Nishati ya Jotoardhi, inayozalisha umeme.
Dk. Mpango, pia akataja kuwa itasaidia kuondoa matumizi ya nishati chafu, akifafanua hitaji lililoko ni nguvu ya ziada kutoka kwa wawekezaji, ili kufanikisha upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu kitaifa.
Raia ya Mkuu huyo wa Nchi Msaidizi ni kwamba serikali isiachiwe pekee jukumu, kwani inaiachia ama kizuizi au ucheleweshaji kupatikana nishati hiyo kwa ajili ya lengo lililokusudiwa.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, serikali imeweka mazingira bora, ikiwamo sera nzuri, sambamba na kuwapo uchumi unaokua kwa asilimia tano, hata baada ya kikwazo cha ugonjwa wa Covid 19.
Anataja kuwapo wataalamu wabobezi katika masuala ya nishati hiyo nchini, hata akatumia nafasi hiyo ya mkutano kuwakaribisha wawekezaji kuendeleza nishati ya jotoardhi katika vyanzo mbalimbali.
VYANZO VINAVYOTATHMINIWA
Dk. Mpango anataja vyanzo hivyo vya majini ni mkoani Mbeya kuna Ngozi (Megawati 70) na Kiejo-Mbaka (Megawati 60); Mto Songwe mkoani Songwe, kunakadiriwa megawati tano hadi 35; Mto Natron, mkoani Arusha (megawati 60; na Ruhoi mkoani Pwani, megawati tano.
Pia, anataja Tanzania imeshakamilisha utafiti wa awali kwenye baadhi ya maeneo matano yenye viashiria vya jotoardhi kwenye Bonde la Ufa na sasa kuna uchorongaji unaoendelea katika eneo la Ngozi, ili kuhakiki uwapo wa nishati hiyo.
Makamu wa Rais, anasema serikali inafanya juhudi kuendeleza nishati ya jotoardhi, kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwamo kuanzisha taasisi maalum ya kusimamia sekta husika, inayopewa jukumu la kusimamia uendelezaji nishati hiyo.
Dk. Mpango anatoa wito kwa viongozi wa Afrika, kuunganisha nguvu zao kushirikiana kufanikisha upatikanaji na matumizi yenye manufaa ya nishati jotoardhi, ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Mtazamo wake wa baadaye mkuu huyo ambaye pia ni mchumi kitaaluma, ni kwamba hazina ya jotoardhi inapotumika vywema, itasadia kuacha matumizi ya nishati zisizo safi katika uzalishaji umeme, ikiwamo mafuta mazito.
Anatoa ushauri kwa kila nchi kuwa na taasisi maalum inayobuniwa kitaifa, kwa ajili ya kusimamia uendelezaji wa jotoardhi, pia kuwa na kanuni na sheria zitakazowezesha sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji nishati hiyo.
NENO LA WADAU
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, George Mkuchika, akaeleza katika mkutano huo kuwa sekta ya nishati inaendelea kupiga hatua chini ya usimamizi mzuri wa serikali na hadi sasa umeme nchini umefika vijijini kwa takriban asilimia 98.
Huku umeme vijijini ukihudumiwa na wakala maalum iitwayo REA, Waziri Mkuchika anataja matarajio yaliyopo ni kwamba ifikapo Desemba ijayo, vijiji vyote nchini vitakuwa vimeunganishwa na huduma hiyo ya umeme.
Mkuchika anasema, hatua ya uendelezaji vyanzo mchanganyiko vya nishati ikiwamo jotoardhi inaongezeka, hali ambayo ikisimamiwa ipasavyo, itasaidia kufikisha malengo yaliyowekwa.
Waziri wa Nishati na Mafuta nchini Kenya, James Wandayi, anahimiza uhamasishaji matumizi ya uzalishaji umeme kupitia jotoardhi barani Afrika, kwa kuwa iko endelevu.
Anataja kwamba zaidi ya asilimia 45 ya umeme nchini humo unazalishwa na jotoardhi, hivyo tayari wanaona mafanikio ya nishati hiyo.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati nchini, Judith Kapinga, akasema jotoardhi nchini ina nafasi ya kuwezesha azma ya serikali kuwa na umeme unaotokana na vyanzo mchanganyiko.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, wamekusudia kutimiza lengo la kuzalisha megawati 995 kwa nishati hiyo, ifikapo mwishoni mwaka 2024.
Anaisifu nishati ya jotoardhi ni suluhisho muhimu katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati ya kutosha barani Afrika, inayoenda sambamba na mipango ya dunia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Naibu Waziri anasema, jotoardhi ina uwezo mkubwa na inabaki kuwa rasilimali maalum kutoka eneo husika, ikitumika na kuunganishwa katika gridi za kitaifa.
Vilevile anataja manufaa yake kwamba, yanaweza kusambazwa kwa usawa kusaidia kukabiliana na tofauti za kijiografia katika upatikanaji nishati, zinazoakisi tofauti kubwa za kiuchumi kitaifa.
Hadi sasa nchini vyanzo vya jotoardhi vinatajwa vipo 52, kwenye mikoa 16, vikitajwa kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme usiopungua megawati 5,000.
Kitaalamu inatajwa, katika usambazaji wa nishati ulio sawa, jotoardhi ina jukumu muhimu katika kushughulikia vipimo vya kijiografia vya ukuaji, ikiwaruhusu raia wengi kushiriki na kufaidika na maendeleo ya kitaifa.
Inatajawa kutokana na umuhimu wa rasilimali hiyo, matarajio yaliyoko ni kwamba mkutano huo utaanzisha suluhisho la kushinda vizuizi vinavyozuia maendeleo ya jotoardhi.
Mbunge George Mwenisongole wa Jimbo la Mbozi akiwawakilisha wabunge wanaotoka kwenye mikoa yenye rasilimali ya jotoardhi, anashauri kuwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye miradi husika, wapewe kipaumbele cha kuhudumiwa umeme.
Mikoa yenye jotoardhi ni Arusha, Dodoma, Iringa, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kagera, Katavi, Shinyanga, Songwe, Manyara, Rukwa, Singida na Tanga.
Mafunzo yaliyotolewa katika kongamano la ARGeo-C10 kuwa ni pamoja na uendelezaji wa vyanzo vya Jotoardhi na teknolojia mpya, athari za masoko ya rasilimali kaboni na matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi katika sekta mbalimbali, ikiwamo kilimo na ufugaji hasa wa samaki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED