MAMBO yanazidi kuiva katika kikao cha kupigania hali ya hewa iboreke duniani, huko mjini Baku, nchini Azerbaijan, nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania zinaona mada zinavyozigusa moja kwa moja.
Kwa namna ya pekee, bendera ya kongole inauangukia Umoja wa Mataifa, mwasisi na mwendeshaji wa vikao hivyo. Kwa ujumla wake, si hoja ya jana wala juzi, ina mzizi wake mrefu, Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa zama hizo akiwa na upekee wake kubuni kitu hicho.
Baada ya kuasisi wazo, alipata shida namna atanavyoinadi na kama itakamilika. Akapangia mkakati kutoka nchi moja hadi nyingine, lakini katika sura yake ya kina wanufaika wakuu, nchi zinazoendelea.
Sasa kinachoendelea, daima hakijawahi kuliacha kundi hilo la dunia, ikiwamo kinachoendelea wakati huu tangu kuanza kikao yapata wiki na nusu sasa.
Akiwa ameshapanga ajenda yake ya ushawishi kati ya bara moja na lingine wakati huo, kila moja ‘akimwingilia’ kulingana na falsafa zake, Ban Ki Moon mnamo katikati ya mwaka 2014, alitua ghafla kisiwani Malabo, mji mkuu wa Guinea ya Ikweta, ambako Waafrika walikusanyika kuteta katika umoja wao, AU.
Ni bahati kamati ya AU inayohusika na hali ya hewa, Mwenyekiti alikuwa swahiba wa karibu wa Ban Ki Moon, Rais Jakaya Kikwete, huku Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshikilia mazingira ni Rais wa sasa, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Ban Ki Moon, alipotua akakutana na kamati hiyo ya Kikwete kwa faragha, akifafanua wamekuwa wakiteta kila mara namna ya kuisuka ajenda kuupata Mkataba wa Paris. Hapo akawaibia siri, Waafrika wachangamke kuiunga mkono.
Akawatumia takwimu namna maendeleo ya viwanda na teknolojia zingine zina athari kubwa ya hali ya hewa kwao Waafrika, wakichangia wastani asilimia 15 na iliyobaki nchi zilizoendelea, lakini wao ndio wanaothirika zaidi.
Ban Ki Moon, akifuatana na rais mtaafu wa Ghana katika ajenda hiyo, akawadokeza kwamba ‘alishamweka sawa’ Rais wa Marekani Barack Obama, kumsaidia kupitisha hilo kwake, naye akiahidi kuwasuka wadau wake wa kisiasa matajiri wamiliki wa viwanda.
“Wabishi ni wale wa Ulaya (EU), lakini nikitoka hapa (jijini Malabo) naenda kukutana nao,” akatamka Ban Ki Moon, akiwaomba Waafrika wamuunge mkono kupitisha hoja kwenye kikao cha kwanza kilichotarajiwa kufanyika jijini Washington, Marekani Septemba mwaka huo (miezi mitatu baadaye).
Hapo ndipo Mwenyekiti Rais Kikwete, aliporejeshewa kipaza sauti kunadi ajenda anayojua kwa kina, awagawie Waafrika wenzake, akiwatamkia wana-kikao: “Sasa Waafrika sikilizeni wenyewe... kila siku nikiwaambiaa mnaleta mawaziri wasio na maamuzi, siku zote tunaishia kuwa na Mengistu (Haile Mariam- aliyekuwa Waziri Mkuu Ethiopia) ... Tupigane!”.
Ni bahati ajenda ilipita kwa hamasa kubwa kikao cha Washington na hata kikao cha Paris, Ufaransa mwaka uliofuata ikahalalisha rasmi kuwa Mkataba wa Paris.
KINACHOENDELEA SASA
Sasa ni miaka tisa, utekelezaji wake unasonga kupitia ajenda za vikao vya kila mwaka vinavyoitwa COP, vikiwa na ajenda za maendeleo makubwa kwa nchi zinazoendelea.
Wakati vikao vinaaza huko Baku wiki iliyopita, kulikuwapo misukumo ya wanaharakati kuyataka mataifa makubwa kutoa pesa za kutimiza malengo hayo, huku ndani ya kikao ikiwa moja ya ajenda muhimu.
Katika mambo ambayo sasa ni muhimu yanajadiliwa, ni ajenda inayoiguisa moja kwa moja Tanzania “‘madini ya kimkakati namna yanagusa tabianchi na mazingira; na kwanini yanaitwa madini yanaitwa ya kimkakati?”
Wakati mkutano huo wa COP29 ukiendelea huko Baku, Azerbaijan, Mtanzania Adam Anthony, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali, anayehudhuria ana ufafanuzi wake.
Anayataja madini hayo ya kimkakati yamekuwa yakitajwa sana kuwa majawabu makuu katika kuhimili na kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Priscilla Lecomte, kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya kibinadamu, ana maelezo yake naye:
“Mimi niko hapa Baku kwa ajili ya kufuatilia zaidi mazungumzo kuhusu madini ya kimkakati au ‘critical minerals’ ambayo ni muhimu sana katika kipindi hiki cha ‘kuhama kwa nishati’, yaani kutoka nishati kisukuku au nishati chafu na kuelekea katika nishati jadidifu au ‘renewable energy’...”
Adam anataja madini hayo ya mkakati kwa Afrika, ikwamo nchini Tanzania ni fursa ya kuhama kutoka nishati chafu, pia kutanua wananchi, akidokeza pia yana changamoto zake, akitaja baadhi; kimazingira, kiafya, haki za binadamu.
Anataja kuguswa sana na Ripoti ya Jopo lililoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, iliyozinduliwa Baku, akinena:
“Imeweka misingi ya namna gani madini ya kimkakati yanaweza kupatikana, jinsi ya kutatua changamoto kwenye sekta ya madini hayo. Mathalani kuongeza thamani ya madini hayo hususan barani Afrika.
“Vilevile, mapendekezo ya kuboresha viwanda vya kushughulikia madini hayo kule yanakochimbwa,” anaesema Adam akisema matumaini yake ni kwamba mapendekezo hayo yatatekelezwa.
Adam anaeleza kuwa Tanzania ina madini mengi ya kimakati, ikiwamo ya grafiti yanayopatikana Kusini, na nikeli yanayopatikana Kaskazini.
“Madini haya ni sehemu tu kati ya orodha kubwa ya madini ya kimkakati ambayo ni sehemu muhimu sana katika kutengeneza nishati, pia katika mapinduzi ya kidijitali,” anasema Adam.
Pia, anafafanua matumizi yake kwa kauli: “Kwa mfano grafaiti na nikeli hutumika katika betri za kuhifadhi nishati kwenye magari ya umeme. Kwenye mapinduzi ya kidijitali ni madini mengine kama kobalti ambayo hutumika kwenye teknolojia ya simu.”
Adam anaendelea “kwenye mkutano kama huu ndio utaweza kuangalia nchi za Afrika zenye madini kama haya zinawezaje kuongeza thamani badala ya kusafirisha tu malighafi.”
HALI YA MAKAZI
Huko huko Baku, kukatoka ufafanuzi kwamba katika nchi zinazoendelea na visiwa vidogo na baadhi ya nchi zenye maendeleo kuna kilio cha kuwapo watu bilioni tatu duniani wanaishi katika mazingira yasiyo rafiki kimazingira.
Mambo ya dharura yanayotajwa yanajumuisha, yamo mipango, uwezeshaji fedha, teknolojia na kujijengea uwezo wa kukabili magumu ya aina hiyo.
Hapo kitaalamu kunaelezwa kwamba, mipango inayoendeshwa ihame kutoka ‘vipande’ na kuhamia katika mfumo mjumuiko unaozalisha mafanikio ya pamoja.
UTALII VS HALI HEWA
Tayari kuna mpango kazi wa Umoja wa Mataifa kupitia COP29 cha nchini, ikilenga sekta muhimu kama vile utalii kuwa na sera zinazoendana na mikakati ya kudhibiti mifumo ya hali ya hewa.
Katika hoja hiyo iliyotengwa siku maalum ya mjadala, inalenga Sekta ya Utalii, ikiangalia mambo kadhaa ya kufanyika katika malengo yake:
Eneo mojawapo ni kuanza na marejeo ya ajenda ya hoja hiyo iliyowahi kupitishwa huko Glasgow, Scotland inataka kuimarishwa hatua katika kuboresha mifumo ya hali ya hewa kitaifa kwa nchi mbalimbali, mifumo ya kujitolea, utawala wake kuimarishwa, huku wadau wakiwa mstari wa mbele kufanikisha ajenda hizo.
Pili, kunasisitizwa kuimarishwa mifumo ya kisayansi katika kushugulikia hali ya hewa na utalii, ikitengenezwa zaidi miundo ya kitakwimu ya Umoja wa Mataifa inayopima uimara wa utalii, ikiendana na mifumo ya gesi ya kijani.
Pia, kuwapo Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu na kujenga ubia katika namna ya uendeshaji wa taasisi hiyo ndani ya mifumo ya chombo hicho cha kidunia, ili itoe matokeo chanya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED