Rais wa Msumbiji atarajiwa kufungua maonyesho Sabasaba

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:48 AM Jul 01 2024
 RAIS wa Msumbiji, Filipe Nyusi.
Picha:Mtandao
RAIS wa Msumbiji, Filipe Nyusi.

RAIS wa Msumbiji, Filipe Nyusi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba Julai 3, mwaka huu.

Pia, anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kukuza biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama.

Akizungumzia ugeni huo jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alisema Rais Filipe anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Samia.

Alisema atakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Rais Nyusi atapokewa na viongozi waandamizi wa serikali na Julai 2, atapokewa rasmi Ikulu ya jijini Dar es Salaam.
 “Wakiwa Ikulu marais hao watafanya mazungumzo ya faragha na rasmi yatakayojikita katika kukuza biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri January, mazungumzo hayo yatafuatiwa na utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano katika sekta za ulinzi, usalama, elimu, nishati, habari na uchumi na kuzungumza na waandishi wa habari.

Alisema pia ziara hiyo inalenga kujadili namna ya kukabiliana na changamoto za kiusalama katika mipaka ya nchi hizo kwa muda mrefu.

“Julai 3, Rais Filipe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya Sabasaba katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam. Kisha atakwenda Zanzibar kwa ziara binafsi na kurejea Msumbiji Julai 4,” alisema.

Waziri huyo alisema ziara hiyo itakuwa ni ya mwisho kwa Rais huyo kama kiongozi wa nchi na atatumia nafasi hiyo kumuaga Rais Samia na Watanzania kwa kuwa atamaliza muhula wa pili wa urais Octoba, mwaka huu, baada ya kuiongoza kwa miaka 10 tangu 2015.

Alisema uhusiano uliendelea kuimarika na mwaka 1977 nchi hizo zilisaini makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo imeshafanya mikutano 15.

“Kupitia mikutano hii, nchi hizi zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama, uhamiaji, biashara, uwekezaji, utalii, kilimo na uchukuzi,” alisema January.

Aidha, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto za kiusalama. Ikiwa ni moja kati ya nchi 11 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilizochangia vikosi vya kulinda amani kutokana na mashambulizi ya vikundi vya kigaidi Kaskazini mwa nchi hiyo, hasa katika majimbo ya Cabo Delgado, Niassa na Nampula.