MTOTO mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane, Martin Ndalu, amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kupigwa shoti baada ya kushika waya uliokuwa ukishikilia nguzo ya umeme katika Mtaa wa CG, Kata ya Kitete, Manispaa ya Tabora.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne saa 2:00 asubuhi.
Alisema mtoto huyo alimtoroka dada yake na kwenda nje na kushika waya uliokuwa umeshikilia nguzo ya umeme na ndipo alipopigwa shoti.
Alisema wakati dada yake akimvuta ili kumwokoa alipigwa shoti akaanguka.
“Walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete, lakini mtoto Martin alifariki dunia na dada yake anaendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri,”alisema Abwao.
Baba wa marehemu, Nyangi Martin, alisema siku ya tukio yeye pamoja na mke wake walikuwa shambani na waliwaacha watoto na dada yao.
Mashuhuda walisema, mara baada ya tukio hilo, wataalamu kutoka Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Tabora walifika eneo la tukio na kutoa waya huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED