Mke adaiwa kuchoma moto nyumba ya mumewe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:43 PM Dec 06 2024
Moto.
Picha: Mtandao
Moto.

MKAZI wa Mtaa wa Mgusu Halmashauri ya Mji wa Geita, Michael Nzumbi hana makazi baada ya nyumba yake kuchomwa moto na anayedaiwa kuwa mkewe kutokana na mgogoro wa kifamilia.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita majira ya asubuhi wakati mwanaume huyo akiwa kwenye ibada kanisani. Inadaiwa kuwa Michael akiwa kanisani, alipigiwa simu na kupewa taarifa kuwa nyumba yake inatetekea kwa moto.

Michael, alisema baada ya kufika nyumbani kwake, aliwakuta majirani na wananchi wengine, wakiendelea kuzima  moto huo.

Alisema jitihada za kuzima moto huo ziligonga mwamba kwa kuwa ulikuwa pia umetekeza  samani, vyakula, mavazi na fedha taslimu zaidi ya Sh.200,000.

Alidai jirani zake ndio waliomtambua mkewe huyo kuwa ndiye aliyechoma nyumba hiyo. Michael, ameiomba serikali kuingilia kati kwa kumchukulia hatua kali kwa mkewe huyo kutokana na kitendo hicho alichodai kuwa ni cha kikatili dhidi yake. 

Alidai mkewe huyo amekwisha kufanya majaribio kadhaa ya kumdhuru kwa nyakati tofauti, ikiwemo kumuunguza kwa kumwagia maji ya moto na kuchoma nyumba hiyo. 

"Mgogoro wangu na mwanamke huyo ulianza muda mrefu zaidi ya mwaka mmoja akinituhumu kuchepuka,” alidai Michael na kuongeza kuwa: “ Baada ya kuchoma hati ya ndoa na kunimwagia maji ya moto  niliamua kumuachia nyumba iliyopo mjini Geita, lakini amekuja tena kuchoma nyumba yangu." 

Baadhi ya mashuhuda, walisema baada ya kufika katika eneo hilo, walikuta nyumba hiyo ikiwaka moto na kulazimika kuvunja mlango na kuanza kuzima kwa kumwagia maji na mchanga.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgusu, Emmanuel Mapalala, alisema baada ya kufika eneo la tukio, alikuta nyumba hiyo ikiwaka moto na kushirikiana na wananchi kuuzima.

"Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia kati ya wanandoa hao, lakini kama kweli mkewe amefanya tukio hili basi serikali ichukue hatua kwani kama angekutwa ndani mwanaume huyo angekufa," alisema.  

Alifafanua kuwa baada ya kufika katika eneo hilo, waliomba msaada kwa mafundi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuzima mfumo wa umeme ili kuruhusu wananchi kuendelea kuzima moto huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja chanzo chake kuwa ni mgogoro wa kifamilia.  Kamanda Jongo, alisema jeshi hilo linamsaka mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya mumewe na kwamba akikamatwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.